Posts Tagged ‘daraja’
‘Daraja Hili … Thamani Yake ni Mvua ya Saa Tatu’
Ndivyo hali ilivyo katika daraja linalounganisha Kinyerezi na Segerea. Ni daraja muhimu kwani linategemewa na maelfu ya wakazi wa upande huo wa Dar es Salaam. Daraja la muda lilijengwa kwa muda wa miezi kadhaa. Malori ya mawe yalimwagwa hapo. Wajenzi wakatumia maarifa yao. Mamilioni ya fedha yaliingia hapo … sijui ni milioni ngapi. Kudumu kwa daraja hilo miezi michache tangu lijengwe kumekomeshwa na mvua iliyodumu kwa saa 3 tu! Hapa ndipo ninakumbuka kauli ya dereva wa daladala aliyetubeba ‘Thamani ya Daraja hili ni saa tatu ya mvua’!
Abiria wengine walijiuliza … ‘hasara hii ni ya nani’? Nani atabeba gharama za ujenzi mwingine wa daraja la muda? Miongoni mwa abiria hakuna aliyekuwa na majibu.
Hapa tunaona umuhimu wa kutumia maarifa yetu vema. Mwezi Desemba 2011 wakati wa mafuriko ya Dar, daraja lililokuwa hapo kwa miaka mingi lilisombwa. Hiyo ilitosha kabisa kutoa angalizo kwa wakandarasi walioshinda zabuni hiyo. Daraja la muda lilipaswa liwe madhubuti na kubwa kuliko lililokuwepo awali, na daraja la kudumu linalopaswa kuwa hapo linatakuwa kuwa kubwa sana, lililopanda juu sana na pana vizuri ili lisije kusombwa na mafuriko.
Tanzania ni yetu sote. Kila mmoja ajisikie uchungu na kuchukua hatua kukabili magumu yanayotusibu!
Ujenzi … Madaraja na Miundombinu
Harakati za ujenzi wa miundombinu zinaendelea katika pande mbalimbali za nchi ya Tanzania. Uzoefu unaonyesha kwamba miradi mingi huwa na viwango vya chini vya ubora. Moja ya sababu za viwango duni ni usimamizi hafifu wa maofisa au mamlaka zinazohusika. Ni kwa sababu hiyo utasikia kwamba barabara imeanza kubomoka mara tu baada ya kukabidhiwa kwa serikali. Mwenendo huu hulitia Taifa hasara kubwa sana, kwani huhitajika fedha nyingine tena ili kukarabati maeneo yale yaliyoharibika.
Kumbe basi, badala ya kuziachia tu mamlaka zinazohusika kusimamia na kukagua miradi hiyo, kila raia wa nchi hii ni vema afungue macho atazame mienendo ya ujenzi wa miundombinu katika maeneo wanayoishi. Pale unapoona dosari fulani, si vibaya kuuliza kwenye mamlaka inayohusika ili wataalamu watoe maelezo ya kiufundi.
Picha mbili hapo juu zinaonyesha ujenzi ukiendelea. Picha hiyo hapo chini ni maandalizi ya ujenzi. Tofauti ninayoona kati ya miradi hiyo miwili hapo juu na huu wa tatu hapa chini ni suala la uzio. Inawezekana wajenzi wa mradi huo hapo chini wana sababu za maana za kujenga uzio kwenye eneo la mradi. Mathalani, huenda ni ili kuimarisha usalama wa mali zao na zana za ujenzi; au pengine wanataka wajenzi wengine wasione teknolojia yao na hivyo ‘kuiiba’ na kwenda kuitumia kwenye mradi mwingine kama huo.
Hata hivyo, na ninakaribisha kurekebishwa, binafsi sioni kama ilikuwa muhimu kuweka uzio. Sana sana mimi naona kwamba utaratibu huo unaweza kuwa na matatizo zaidi kuliko manufaa. Kwa mfano, hapo kuna hiyo kali katika barabara nyembamba ya muda na kuna daraja dogo. Uzio unatengeneza ‘blind spot’ hapo gari linapokaribia daraja. Kwa hiyo, ni rahisi kwa ajali kutokea na hatujui itasababisha hasara zipi! Lakini pia, huu kama mradi wa umma sioni kwa nini uzibwe ili watu tusione — je, wajenzi hawataki tuone ni aina gani ya nondo zinaingia kwenye daraja? Ni kiasi gani cha nondo kinahitajika kutumika?
Nafikiri wananchi tuna haki ya KUONA na kutathmini. Hatutaki tuje tushtukizwe baadaye na uduni wa daraja. Inafaa kuona ili kama ni kulaumiwa, tulaumiane sisi wenyewe kwa kutochukua hatua zinazostahili mapema.
Nawasilisha hoja. Pamoja sana.
Segerea Darajani … Uvukaji
Baada ya daraja lililokuwepo kusombwa na mafuriko miezi michache iliyopita … hivi ndivyo baadhi ya magari na watu wanavyovuka bonde hili. Ni katika Mto Msimbazi, sehemu inayounganisha Segerea (upande wa Seminari) na Sitakishari (Majumbasita).
Mahali lilipokuwa daraja kabla ya kusombwa. Chora mstari wa moja kwa moja na barabara iliyo ng’ambo ya mto (bonde la mto).
Bonde la mto baada ya kupanuliwa na mmomonyoko wa udongo …
Upande mwingine wa bode … nyumba zilizokuwa karibu kusombwa na maji.
Swali la kizushi
Mamlaka inayohusika na barabara hii … daraja hili litajengwa lini? Kimsingi, barabara hii inafupisha sana umbali kati ya Segerea na Sitakishari hadi Uwanja wa Ndege. Vilevile, endapo kuna tatizo lolote katika barabara ya Kinyerezi-Majumbasita, hii inaweza kutumika. Kumbe, ni barabara muhimu na yafaa kwamba daraja litengenezwe upya. Pamoja … sana.