Posts Tagged ‘ajali’
Treni ya Mwakyembe … Madereva Kaeni Chonjo
Garimoshi la abiria wa Dar es Salaam likiwa katika moja ya safari zake kati ya Posta na Ubungo Maziwa.
Gari dogo la binafsi likiwa kwenye moja ya foleni za magari jijini. Hata hivyo, gari hilo lipo katikati ya njia ya reli.
WAKATI ambapo wakazi wa baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam wanaendelea kunufaika na kuanzishwa kwa usafiri wa abiria wa ndani ya jiji (Commuter train) — tangu katikati ya mwezi Oktoba — kuna haja tupeane hadhari.
Njia ya reli inayotumika kwa usafiri huu wa aina yake — asante kwa juhudi za Dkt Harrison Mwakyembe, Waziri wa Uchukuzi — inakutana na barabara kuu na ndogo na hata njia na vijia vingi sana. Katika baadhi ya makutano hayo kuna wasimamizi na vizuizi vilivyoanziswa, hata hivyo kuna mahali pengi ambapo hakuna watu na nyenzo hizo. Kumbe basi, badala ya madereva na waenda kwa miguu kutegemea tu nyenzo hizo pamoja na king’ora cha garimoshi, ni vema tukajifunza kuheshimu sehemu hizo za makutano na kuongeza uangalifu na umakini.
Binafsi sioni kwa nini mtu unayeendesha gari ulisimamishe kwenye njia ya reli. Hebu fikiri kama garimoshi litatokea ghafla, utafanya nini wakati mbele na nyuma na pembani kote umebanwa na magari? Hivi, unapoteza nini kwa kusimamisha gari lako walau mita tatu kutoka njia ya treni?
Inafaa tujifunza kuepuka ajali zisizo za lazima. Tuache kumjaribu Mungu (na bahati mbaya). Tufuate kanuni ya ‘akili ya kuzaliwa nayo’ (common sense). Si lazima Dkt Mwakyembe aje kusimamia na jambo hili.
Vivyo hivyo kwa waendesha pikipiki, baiskeli, mikokoteni, bajaj na hata waenda kwa miguu … umakini tuwapo barabarani saa zote utatusaidia sana kupunguza ajali, hasa kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.
Nawakilisha. Pamoja sana.
Ajali … Kinyerezi
Ni ya uso kwa uso … Hiace na Lorry
Viti vya kwenye Hiace … viliparaganyika na vingine kung’oka
Mparaganyiko wa viti kwenye daladala …
Barabara ilifungwa kwa muda … kisha magari yalianza kupita upande mmoja wa barabara kwa kusubiriana
Ni majira ya saa 2 usiku. Wakati ninawasili eneo la tukio, kiasi cha kama dakika kumi zilikwishapita. Ni basi dogo, Hiace, na lorry la kama tani tatu yaliyohusika na ajali hii. Magari haya kwa yanavyoonekana, yaligongana uso kwa uso. Baada ya kutazama, inaelekea kwamba dereva wa lorry ndiye aliyehama kutoka upande wake wa barabara na hatimaye kugongana na daladala hilo. Baadhi ya abiria waliokuwa kwenye daladala hilo bado wapo. Wengine bado wana mshtuko wa kuhusika kwenye ajali. Wananieleza kwamba walioumia hasa ni madereva wote wawili wa magari hayo. Madereva hao hawapo hapo lakini wamekwishatoka, hakuna aliyejua hasa wako wapi. Lorry lilikuwa likiteremka kwenye kilima kutoka upande wa Kinyerezi na Haice ilikuwa ikipanda kilima hicho kutoka Njia Panda Segerea.
Ajali. Barabara ni nyembamba na ina miteremko mikali kidogo na madaraja daraja. Ingawa hakuna aliyepoteza maisha katika tukio hili, lakini mtu unapata maswali mengi. Linaloumiza kichwa zaidi ni kuhusu umahiri wa madereva wetu hapa nchini. Ajali zilizo nyingi zinasababishwa na uzembe wa madereva. Mtu unajiuliza, hivi hizi leseni zilizo mikononi mwa madereva … wanazistahili kweli? Je, vigezo vyote na masharti yalizingatiwa kabla ya kuwapa leseni hizo? Je, polisi wa usalama barabarani wanafanya kazi yao kikamilifu … au ndiyo baadhi wanawalinda wahalifu wa makosa ya barabarani baada ya kulambishwa shilingi mbili tatu?
Tupige vita ajali. Tunaweza kuwa na barabara zilizo salama katika nchi yetu. Kila mmoja atimize wajibu wake vizuri. Pamoja sana!
Changamoto za maisha … vijijini
Afya. Gari la wagonjwa likiwa limekata chuma kinachounganisha gurudumu la mbele. Safari ilikomea hapo. Kwa bahati umbali kufika mjini ulibaki kama km 25 hivi, kwa hiyo mgonjwa alimalizia safari yake kwa gari lingine lililokuwa likipita hapo.
Maji. Miundombinu bado ni hafifu. Hivi ni kipi kinachotuzuia kutumia miundombinu kama hii iliyowahi kujengwa tangu miaka ya nyuma? Kwa nini wananchi waachwe kuendelea kuteseka kwa kwenda kutafuta maji mbali wakati tenki kama hili lingewapunguzia adha hiyo?
Kipato. Ni vigumu kuendesha maisha ya maana pasipo kipato cha uhakika. Je, vipi kuhusu haki za mtoto aliye mgongoni hapo? Nchi ina wajibu wa kuleta mabadiliko ya maana kwa wananchi kama huyu.
Elimu. Katika maeneo mengi hakuna madarasa ya maana. Kwa hiyo, hata watoto wanapofika umri wa kwenda shule hakuna mahali wanapoweza kwenda. Katika kijiji kimojawapo kuna vijana walioamua kujitolea kufundisha watoto. Kila mzazi anapaswa kulipa walau Sh1,000 kwa mwezi. Hata hivyo, wengi huwakatisha watoto wao masomo kwa kushindwa kumudu kiwango hicho … au pengine kwa kutoipa elimu kipaumbele. Hamasa na elimu kwa watu wazima ni muhimu ili watoto wapate fursa nzuri zaidi za kusoma.
Vitabu. Uhaba mkubwa. Kwenye darasa hilo kulikuwepo vitabu viwili tu. Mahitaji ya elimu yatakidhiwa vipi kwa mwendo huu? Kiu cha elimu ni kikubwa. Ukame wa vitabu, madarasa, walimu, madawati na vifaa vingine ni mkubwa mno.