simbadeo2000

WAZA MPAKA BASI (THINK TO NO END).com weblog NOTE: Views or opinions expressed in this blog do NOT in any way represent those of any organisation, community, association, company, circle of friends, religious or ethnic group to which I am associated with.

Archive for December 9th, 2008

Uhuru Day

leave a comment »


dscf00141

 

dscf0016

Tanzania imeadhimisha miaka 47 ya uhuru wake leo. Juu ni mnara wa uhuru katika viunga vya mapumziko vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam. Chini ni uhaba wa habari juu ya Sikukuu ya Uhuru katika magazeti kwenye kurasa zao za mbele. Ni gazeti moja tu, la The Citizen, ndilo lililobeba habari ndogo juu ya siku hii muhimu kwa Taifa letu.

Yapo mengi ya kujiuliza. Umri wa miaka 47 ni  umri mkubwa. Je, Tanzania imesonga mbele au imerudi nyuma katika maendeleo yake na ya wananchi wake? Mpaka katikati ya miaka ya 70 tulikuwa na viwanda vinavyozalisha bidhaa mbalimbali: zana za kilimo, redio, nguo, viatu, baiskeli, vipuri na mambo kadha wa kadha. Leo hii viwanda hivyo havipo au vimekwishabinafsishwa na kubadilishiwa matumizi. Vingine vimekuwa mabohari tu na vingine vinafanya shughuli nyingine ambazo ni vigumu kuziunganisha na dira yetu ya maendeleo kwa ujumla.

Wakati huohuo, jeshi la watu wasio na ajira rasmi na zenye mwelekeo wa kuzalisha kwa ajili ya maendeleo yao na yale ya Taifa linazidi kuwa kubwa. Kila mwaka wanazalishwa vijana mamia elfu wasio na uhakika wa ajira ya kudumu. Kilimo tunazidi kukitupa mkono, elimu inazidi kuwa ‘bora elimu’ na si ‘elimu bora’, maradhi (UKIMWI, malaria, TB, na mengine mengi yanazidi kushamiri. Miundo mbinu bado ni kitendawili – usafiri wa reli, anga, barabara na hata majinibado ni wa ubora wa chini.

Tujiulize iweje badala ya kuendelea kuwa wazalishaji tunazidi kugeuzwa kuwa dampo la kuuzia bidhaa, tena zilizo nyingi zikiwa ‘feki’, hivi sisi Watanzania tunafanya nini? Au ndiyo tuseme sote tumelewa ‘harakati za kujitafutia’ utajiri kwa njia za haraka na za kijanjajanja?

Hima tuamke. Turejee tafakari ya Rais J.F. Kennedy: Jiulize umeifanyia nini nchi na si nchi inakufanyia nini. Mjenga nchi ni mwananchi na mbomoa nchi ni mwananchi.

Written by simbadeo

December 9, 2008 at 11:27 pm

Posted in Siasa na jamii