simbadeo2000

WAZA MPAKA BASI (THINK TO NO END).com weblog NOTE: Views or opinions expressed in this blog do NOT in any way represent those of any organisation, community, association, company, circle of friends, religious or ethnic group to which I am associated with.

Posts Tagged ‘ajira

Ajira: Wanawake na Maendeleo

leave a comment »


Wanawake na Maendeleo

Ajira rasmi bado ni changamoto kubwa kwa nchi yetu. Kwa mujibu wa matokeo ya ‘Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa Mwaka 2014’ wa National Bureau of Statistics, kuna jumla ya watu 25,750,116 wenye uwezo wa kufanya kazi nchini. Miongoni mwao, Nguvu Kazi ya Taifa ni 22,321,924. Na kati ya hao kwenye kundi hilo la pili, walio kwenye ajira ni 20,030,139. Idadi hiyo ni jumla ya walio kwenye ajira rasmi na isiyo rasmi.

Kwa mujibu wa utafiti huo, sekta isiyo rasmi haijumuishi shughuli za kilimo. NBS inafafanua kuwa ni zile shughuli za kiuchumi zinazofanywa na mtu mmoja mmoja au na kaya lakini ambazo ni vigumu kisheria kuzitofautisha na wamiliki wake, kwani mara nyingi hazina akaunti zake zenyewe za benki, baadhi ya bidhaa wanazozalisha ni kwa ajili ya kuuza huku zikiajiri chini ya wafanyakazi watano.

Utafiti huo unaonyesha kuwa kuna kaya 4,338,070 zenye shughuli za kiuchumi zilizo katika sekta isiyo rasmi. Lakini utafiti unaonyesha kuwa wanaofanya kazi mmojammoja katika sekta isiyo rasmi ni watu 6,257,124.

Kwa hiyo, nchi yetu ina changamoto kubwa ya kuwaingiza hawa katika sekta rasmi. Ni kwa sababu ya ukosefu wa ajira rasmi siku hizi tunaanza kuona akina mama wakifanya shughuli za uchuuzi mijini. Shughuli hizi zilikuwa zikifanywa zaidi na akina baba. Hii ni kwa maana ya kubeba bidhaa na kuzitembeza kutafuta wateja.

Tulipe kodi ili kwa pamoja tulete mabadiliko katika uchumi wa nchi yetu.

Pamoja sana.

Advertisements

Magufuli: Tazama eneo hili pia

leave a comment »


Biashara ndogondogo Chalinze 1

Chalinze. Wachuuzi wengi ni wanaume.

Soni Akina mama wafanyabiashara

Soni, Lushoto. Wachuuzi wengi (kama sio wote) ni akina mama.

Mazao Biashara Ndogondogo 2

Mazao ya shamba. Masoko bora zaidi yanahitajika.

 

Ajira. Uchumi wa nchi hauwezi kukua endapo nguvukazi haitatumika vema kwa namna yenye kuleta tija kwao na kwa nchi. Wachuuzi walio hapo juu wanajitafutia riziki. Kile wanachopata hakiendani na nguvu wanayotumia. Tukiwa na utaratibu mzuri wa masoko — yaani kutafuta masoko ya uhakika — hawa watapata kipato kizuri zaidi. Hapo walipo ni vigumu kwao kulipa kodi (kama wanalipa basi ni ushuru kidogo unaokwenda halmashauri). Lakini wakiwa katika masoko maalumu, watapata kipato kizuri na kulipa kodi.

Mazingira wanayofanyia biashara pia si rafiki. Ni muhimu kubadili hali hii. Hivi sasa tunachokiona hapo juu kipo karibu kila kona, kila mji, kila njia kuu nchini Tanzania. Ni muhimu tubadili hii. Tunaweza tu kwa kufanya uchumi wetu ujiendeshe kwa nia zilizo rasmi. Kilimo kifanywe kwa tija na kwa njia zilizo rasmi, biashara ifanywe kwa njia rasmi. Serikali ifanye kazi kutafuta masoko ya uhakika kwa bidhaa zote zinazozalishwa nchini — za kilimo, mifugo, bahari, maziwa, mito na madini.

Ajira rasmi. Masoko ya uhakika. Kipato bora. Kulipa kodi. Kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara (ikiwemo miundombinu). Haya ndiyo baadhi ya mambo yatakayoleta mabadiliko chanya katika maisha ya Watanzania.

Pamoja sana.

Mshangao. Pale Chalinze wachuuzi ni wanaume (zaidi), kule Soni ni wanawake (zaidi). Sina majibu kwa hali hii. Je, Chalinze wanaotoka ni wanaume, wanawake wanabaki nyumbani? Je, kule Soni wanaotoka ni wanawake, wanaume wanabaki nyumbani? Kwa anayejua atujuze. Nafikiri kuna kitu cha kujifunza hapa.

Kazi: Pengine ya kwako ni ngumu, tazama ya hawa…

leave a comment »


SAM_8637

Naam. Hii ni hatua ya katikati. Maana kazi yenyewe huanzia na kuangusha miti, kukata magogo na kisha kutengeneza matanuri. Ndugu huyu hapa anahakikisha kuwa tanuri la mkaa linaendelea vema.

 

SAM_9144

SAM_9146

Hatua nyingine ni usafirishaji. Kuna wanaobeba kwa vichwa, baiskeli, pikipiki na hata malori. Tafakari ugumu wa kazi ya wachoma mkaa. Linganisha na kazi yako. Huenda unalalamika kuwa kazi yako ni ngumu. Je, ni ugumu wa aina hii? Vipi kuhusu kipato kinachotokana na kazi yao, unakilinganisha vipi na cha kwako kwa kazi yako?

Angalizo

Wakati huohuo, ni muhimu tufanye jitihada kwa jamii yetu ya Watanzania ili tutoke katika matumizi ya mkaa. Yanaua mazingira. Yanaua maendeleo. Yanaua afya. Sasa tuna gesi. Tuhakikishe kwamba kila mmoja wetu anamudu gharama za gesi pamoja na zana zinazotakiwa ili tuhifadhi miti na misitu yetu.

Pamoja sana.

Zege Halilali … Mwendo Unabadilika

leave a comment »


Dar Roads

Mwendo unabadilika. Siku hizi yameingia malori yanayofanya kazi ya kuchanganya zege kwa ajili ya ujenzi wa majengo makubwa. Hapo kabla bado vijana ndivyo walikuwa wanapata kazi hiyo ya kuchanganya zege. Bado hata hivyo wanaendelea kupata kazi hizo. Isipokuwa, kadiri siku zinavyokwenda … malori haya yanaongezeka na hii inahatarisha ajira za vijana. Ni hali tete. Lakini pamoja na kwamba malori haya yanakuja kuchukua nafasi za kazi za vijana hao, yenyewe yanafanya kazi kwa ufanisi zaidi na kwa muda mfupi zaidi.

Pengine ingefaa wizara inayohusika — Ajira na Maendeleo ya Vijana — kuhimiza njia mbadala za vijana kujipatia ajira hasa kulingana na mabadiliko ya teknolojia. Miaka ya nyuma kidogo ulimwengu ulitishika kwamba computer zilikuwa zinakuja kunyang’ganya watu ajira … hivi sasa computer hata huku kwetu zina zaidi ya miaka 20 na bado watu wanapata ajira.

Kwa hiyo, hatuna budi kama jamii kubadilika kuendana na teknolojia … lakini ni muhimu kujifunza njia mbalimbali za kufanya kazi na kuweza kujiajiri. Kilimo ni sekta moja muhimu sana … Vijana wafundishwe namna ya kumudu mitambo hii na mingine katika kilimo na nyanja mbalimbali za uchumi.

Pamoja sana.

Written by simbadeo

December 7, 2012 at 12:54 am

Dar Mitaani … Siamini Macho Yangu

leave a comment »


Kama siamini macho yangu vile! Tunaanza kuona kazi za sanaa kwenye mitaa ya Darisalama. Hizi ni katika Mtaa wa Makunganya, katikati ya jiji. Kwangu ilikuwa mshtuko kidogo … maana mambo haya hatukuzoea kuyaona hapa. Nipongeze mamlaka inayohusika na mpango huu. Ni mwanzo mzuri na hauna budi kuendelezwa. ILA tafadhali sana tuwashirikishe wanasanaa wa hapa nchini katika kufanya kazi hizi. Wao ndiyo wanaofahamu vema kabisa vionjo vya Watanzania. Kwa kuwahusisha wao, ni njia ya kukuza kazi za sanaa hapa nchini ili zipate kuthaminiwa kama zinavyostahili.

Kupitia sekta ya sanaa, nchi itapata fursa ya kukuza na kudumisha utamaduni wake; itazalisha nafasi nyingi za ajira; itachangia kuongezeka kwa kasi ya kukua kwa uchumi; itaimarisha thamani ya mwanadamu na ubinadamu na hata kukuza viwango vya kufikiri, namna ya kupanga vipaumbele katika maisha na mipango yetu ya mtu mmoja mmoja na ile ya Taifa — yaani katika kutazama hasa substance na si accident. Pamoja sana!

Written by simbadeo

September 2, 2012 at 11:00 pm

Posted in Siasa na jamii

Tagged with , , , ,

Katika Kituo Kikuu cha Mabasi … Singida

leave a comment »


Hali hii hivi sasa inaonekana karibu katika kila kituo cha mabasi ya safari ndefu na fupi. Majeshi ya vijana — wake kwa waume — wakichuuza bidhaa mbalimbali kwa kuzibeba mikononi. Kwa kweli ni hali ya hatari. Sina hakika kama biashara za mtindo huu zina tija yoyote kwa Taifa na hatma yake. Tujitafakari. Tutengeneze ajira zenye hadhi kwa vijana wetu ili tujenge Taifa madhubuti, lenye viwango vya juu vya uzalishaji vitakavyousukuma mbele uchumi wetu na kuupa nguvu ya kujitegemea. Kwa maoni yangu, badala ya wasomi kukimbilia kwenye siasa, kila aliye na shahada ya uzamiri ipitishwe sheria kwamba atengeneze nafasi za ajira zenye hadhi zisizopungua 10, na wale wenye shahada ya uzamivu watengeneze ajira zenye hadhi zisizopungua 50. Pengine hivyo navyo viingizwe kuwa vigezo vya kupata shahada hizo. Vinginevyo Taifa halina tija na shahada zinazobaki kwenye magamba yanayoning’inizwa ukutani au kufichwa sandukuni. Nawasilisha.

Written by simbadeo

August 2, 2012 at 1:38 am