simbadeo2000

WAZA MPAKA BASI (THINK TO NO END).com weblog NOTE: Views or opinions expressed in this blog do NOT in any way represent those of any organisation, community, association, company, circle of friends, religious or ethnic group to which I am associated with.

Margaret Thatcher … Afariki Dunia

leave a comment »

Margaret Thatcher

Margaret Thatcher

Margaret Thatcher

Margareth Thatcher


MARGARET THATCHER AFARIKI

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke wa Uingereza, Bibi Margaret Thatcher, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 87. Alizaliwa mwaka 1925. Amefariki ‘kwa amani’ baada ya kupata ugonjwa wa kiharusi (tangu mwaka 2002), familia yake imesema.

Waziri Mkuu David Cameron amemtaja kama “raia mwenye mchango mkubwa katika Uingereza” huku Malkia Elizabeth akieleza kuwa amehuzunishwa mno na kifo hicho.

Bibi Thatcher, aliyejulikana kwa jina la utani kama ‘Iron Lady’, yaani bibi mwenye msimamo mkali kama chuma, alikuwa Waziri Mkuu kutoka chama cha Conservative kati ya mwaka 1979 hadi 1990.

Imetangazwa kwamba hakutakuwa na mazishi ya kitaifa bali atapewa heshima sawa na ile aliyopewa Princess Diana na Mama Malkia. Bendera ya Ufalme wa Uingereza katika Ofisi za Waziri Mkuu Namba 10 Mtaa wa Downing inapepea nusu mlingoti.

Je, kifo hiki kimepokelewa vipi mahali mbalimbali duniani?

Rais wa Marekani, Bw Barack Obama amesema: “Kwa kifo cha Bibi Margaret Tatcher, dunia imempoteza mmoja wa watetezi
wakubwa wa uhuru na haki ya kuchagua mtindo wa maisha, na Marekani imempoteza rafiki wa kweli. Akiwa binti wa mwuza duka aliyefikia hata ngazi ya kuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke, anakuwa mfano kwa mabinti zetu kwamba hakuna ‘dari la kioo’ lisiloweza kuvunjwa. Katika nafasi yake kama waziri mkuu alichangia sana kurejesha imani na kujivuna sifa ambazo daima zimekuwa kilelezo cha Uingereza kama taifa bora kabisa. Na kama mwunga mkono asiyeyumba wa mshikamano wa pande mbili za bahari ya atlantiki, alijua kwamba kwa msukumo na nia thabiti tungeweza kushinda Vita Baridi na kueneza ahadi ya uhuru kila mahali.

Hapa Amerika, wengi wetu tunakumbuka vema taswira zake akiwa amesimama bega kwa bega na Rais Reagan, wakiikumbusha dunia kwamba hatukuwa tu tukisombwa na mawimbi ya historia — bali tumekuwa waundaji wake kwa kuwa tumejishawishi na kuamini pasipo na shaka, ujasiri mkuu na ulio imara.

Michelle na mimi tunapeleka salamu zetu za rambirambi kwa familia ya Thatcher na raia wote wa Uingereza tunapoendelea kufanya kazi ambayo alijitoa kuifanya kwa moyo wote ya kuwakomboa watu, kuwaunganisha na kwa pamoja kuazimia kuandika historia yetu wenyewe.”

Kutoka Nchini Argentina. Vita kati ya Uingereza na Argentina ilipiganwa Margaret Thatcher akiwa waziri mkuu, mwaka 1982. Nchi hizo zilikuwa zikigombea Visiwa vya Falklands vilivyo karibu kabisa na Argentina, huku
kila upande ukidai kuvimiliki. Roberta Radu wa Argentina anasema: “Hiki ndicho Ernesto Alberto Alonso, rais wa kitaifa wa kamisheni ya wanajeshi waliopigana kwa ajili ya visiwa vya Malvinas (ndivyo vinavyojulikana visiwa hivyo nchini Argentina), alisema: ‘Kama ambavyo mtu yeyote anapofariki, nilianza kwa kutafakari mafanikio na upungufu wa Waziri Mkuu. Mwanamke huyu alikuwa mtu aliyesababisha matatizo siyo nchini mwake tu bali hata katika ngazi ya kimataifa. Nitamkumbuka daima kama kiongozi ambaye hakuwa na mchango katika amani ya dunia. Kwa namna nyingi, ninamfananisha na utawala wa kidikteta wa kijeshi uliokuwa hapa, na hasa ule wa Galtieri. Atakumbukwa kama kiongozi ambaye hakutoa mchango wowote wa maana kwa umma wa watu’.

Aliongeza kusema kuwa, wakati huu yeye yuko na wapiganaji wengine wa zamani wakisaidia juhudi za uokoaji kufuatia mafuriko ya La Plata, na alishangazwa na habari hizi za kifo. Wapiganaji wengine wanakubaliana naye na kusema “hakuwa mtu mwema”.

Jinsi kifo kilivyopokewa kwenye Visiwa vya Falkland

Mwananchi wa Visiwa hivyo, Rosie King, ambaye ameishi katika mji wa Port Stanley tangu kabla ya vita mwaka 1982 alisema: “Kama ilivyo kwa visiwa vingi hapa ambavyo husherehekea Siku ya Bibi Thatcher kila Januari 10, mwanamke huyu anaonekana kuwa shujaa hapa.

“Pengine yeye ni mtu nambari moja katika historia yetu. Tumepokea habari hizi kwa huzuni ubwa ingawa ni jambo lililotarajiwa kwa sababu tulijua kwamba alikuwa na afya isiyo njema. … Kwa hakika hapa kutakuwa na misa maalumu ya kumkumbuka na bendera zitapepea nusu mlingoti.”

“Nilikuwa na umri wa miaka 25 wakati wa vita. Ilikuwa jambo la kuogofya sana tuliposikia kupitia matangazo ya redio kwamba Thatcher angetuma kikosi maalumu. Na baadaye yeye mwenyewe alipowasili, ilikuwa kama vile ni Malkia mwenyewe ndiye aliyekuja.”

“Nilikutana naye kwenye moja ya kona za mitaani, na tuliongea kirafiki kabisa. Alivaa hali ya kawaida na si kama mmoja wa viongozi wakubwa duniani. Hakuwa na ule ukali kama ambavyo mara nyingi alichukuliwa kuwa nao, na alikuwa mdogo kuliko nilivyofikiri… Ilikuwa ni moja ya vipindi vya pekee vya kukumbuka katika maisha yangu.”

Na hii ni kutoka kwa FW De Klerk, aliyekuwa Rais wa Afrika ya Kusini (enzi za utawala wa Ubaguzi wa Rangi).
“Nimepokea kwa huzuni kubwa kifo cha Bibi Thatcher. Atakumbukwa siyo tu kama mmoja wa Mawaziri Wakuu wakubwa kabisa katika historia ya Uingereza bali kama kiongozi aliyekuwa na sera na mitazamo ambayo ilikuwa na mchango mkubwa duniani kote.

Ingawa alikuwa daima mkosoaji wa siasa za ubaguzi wa rangi (Apartheid), yeye alielewa vizuri zaidi hali halisi changamano iliyokuwa ikiikabili Afrika ya Kusini pengine kuliko viongozi wengine wengi wa enzi zake. Daima, na kwa usahihi kabisa, aliamini kwamba kungekuwa na mafanikio zaidi kupitia ushikiano wa kujenga pamoja na serikali ya Afrika ya Kusini kuliko kuweka vikazo vya kidhalimu na kuitenga. Pia alielewa na kuona umuhimu wa kushughulikia madai na matashi ya watu wote wa Afrika ya Kusini katika kutafuta maelewano ya kikatiba.

Ni kwa sababu hii kwamba aliweza kuwa na mchango wa pekee yakinifu katika kusaidia mchakato wetu wa kuleta mageuzi ya kikatiba yasiyojikita kwenye ubaguzi nchini Afrika ya Kusini. Tangu mkutano wangu wa kwanza na yeye jijini London baada ya kuchaguliwa kwangu kama kiongozi wa National Party mwaka 1989 na katika kipindi chake chote cha kumalizia uongozi wake kama Waziri Mkuu, alitoa msaada wa maana kwangu na kwa viongozi wengine katika kutafuta Afrika ya Kusini yenye amani, ustawi na inayoendeshwa kikatiba.

Tulikutana kwenye majiji ya Cape na London mara nyingi baada ya kustaafu kwake — na kabla ya kupatwa na kiharusi mwaka 2002. Ninajisikia fahari kwamba Margareth Thatcher alikuwa rafiki yangu.”

Swali

Je, Hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere angalikuwa hai angemwelezea vipi ‘Iron Lady’? Kwa ujumla, tunaelewa kwamba Nyerere alikuwa na misimamo mikali sana hasa dhidi ya utawala dhalimu wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika ya Kusini. Mwalimu Nyerere aliigeuza Tanzania kuwa kituo kikuu ya kupiga vita ukoloni mkongwe, ukoloni mamboleo na ubaguzi wa kila aina. Tanzania ilikuwa mstari wa mbele katika kukomboa mataifa mengi yaliyo kusini mwa Afrika. Kwa sababu hiyo, yeye alitofautiana sana na Bibi Thatcher kwa sababu nyingi. Je, angesema nini? Huzuni kwa kuwa aliyefariki ni binadamu.

Blogu hii inatoa pole kwa familia ya Waziri huyo Mkuu wa zamani wa Uingereza. Wakati huohuo tunasema kwamba viongozi wetu — wakuu kwa wadogo — watahukumiwa na historia katika namna walivyotumikia madaraka yao.

Pamoja sana.

Chanzo cha habari na Picha: BBC World News

Advertisements

Written by simbadeo

April 8, 2013 at 6:55 pm

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: