simbadeo2000

WAZA MPAKA BASI (THINK TO NO END).com weblog NOTE: Views or opinions expressed in this blog do NOT in any way represent those of any organisation, community, association, company, circle of friends, religious or ethnic group to which I am associated with.

Archive for March 6th, 2013

Hugo Chavez … Kifo Chake Chapokelewa kwa Hisia Kubwa

leave a comment »


Rais Hugo Chavez wa Venezuela enzi za uhai wake ...

Rais Hugo Chavez wa Venezuela enzi za uhai wake …

Hugo Chavez 1

Wafuasi wa Chavez wamiminika mitaani wakiomboleza kwa hisia kali

Wafuasi wenye simanzi kubwa na ambao wamepigwa na bumbuazi kufuatia kifo cha Rais wa Venezuela Hugo Chavez walimiminika kwenye mitaa Jumanne wakilia, wakiimba kauli mbiu mbalimbali huku wakijiapiza kuendelea kumuenzi shujaa wao wa mapinduzi.

Huku wakikusanyika mitaani na kwenye viwanja vya wazi katika taifa hilo la Bara la Amerika ya Kusini lenye jumla ya watu milioni 29, waungaji mkono wa kiongozi huyo wa kijamaa walipaaza sauti: “Chavez ataishi milele!” na “Mapambano yanaendelea!”

“Lazima tuonyeshe kwamba yale aliyotenda hayakuwa bure,” alisema Jamila Rivas, 49, aliyekuwa akilia kwa kuomboleza nje ya hospitali ya kijeshi ambamo Chavez aliaga dunia. Mamia ya wafuasi walimiminika kwenye hospitali hiyo.

Raia wa Venezuela wamekuwa wakifuatilia kwa karibu kupanda na kushuka kwa afya ya kiongozi wao kwa kipindi cha miaka miwili ambapo amekuwa akipambana na saratani. Hata hivyo, wafuasi wake wengi walikuwa kama hawaamini kwamba kiongozi wao huyo mahiri na shupavu alikuwa amewatoka.

“Alikuwa baba yetu. ‘Uchavez’ hautaisha kamwe. Tutaendelea kupambana!” alisema Nancy Jotiya, 56, jijini Caracas’ katika viwanja vya wazi vya Bolivar, ambavyo vilipewa jina la shujaa wa uhuru wa Venezuela na ambaye Chavez alimhusudu sana, Simon Bolivar.

“Nilimuhusudu. Alikuwa mtu mwenye moyo mkubwa,” alisema mama mmoja wa nyumbani Aleida Rodriguez, 50, ambaye alipata taarifa wakati akitoka kwenye mfumo wa usafiri wa chini ya ardhi.

Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela Henrique Capriles alituma salamu zake za rambirambi na kutoa wito wa umoja nchini humo.

Rais Hugo Chavez anaondoka katika kipindi ambapo taifa lake limegawanyika vikali kati ya wafuasi wake yeye mwenyewe na wale wa upinzani. Upande wa upinzani ulimtangaza Hugo Chavez kama dikteta mkubwa na aliyekandamiza haki za kidemokrasi.

Lakini upande wa wafuasi wake umemchukulia kama kiongozi makini, anayepigania maendeleo ya watu wa kawaida na aliyelitetea taifa hilo dhidi ya unyonyaji na ukandamizaji unaofanywa na taifa la Marekani mahali pengi duniani.

Hayati Hugo Chavez atakumbukwa kama kiongozi mwana harakati katika siasa na masuala ya kimataifa. Alilichukulia taifa la Marekani kama adui nambari moja. Mara kadhaa katika kampeni zake, hotuba zake na maongezi yake alidhihirisha upinzani wake mkubwa kwa ubabe wa taifa hilo kubwa duniani. Kwa sababu hiyo, alijipatia waungaji mkono wengi kutoka pembe mbalimbali za dunia na hasa kutoka mataifa yanayoendelea. Kwa hakika kifo chake kitakuw pigo kwao hasa kwa sababu wanapoteza mtu aliyethubutu kuikabili Marekani na kuieleza hisia zake pasipo kuogopa.

Blogu hii inaungana na raia wa Venezuela kuomboleza kifo cha kiongozi huyo mashuhuri atakayekumbukwa kwa uzalendo wake wa kupigania maslahi ya raia wa nchi yake. Kwa hakika alikuwa kiongozi wa kupigiwa mfano na viongozi wengi — hasa barani Afrika. Uzalendo, kupigania haki za wanyonge, kujaribu kuleta usawa, kupigania maendeleo ya kila mmoja ni baadhi ya mambo ambayo kwayo watu wengi walimhusudu kiongozi huyu. Pamoja sana!

Chanzo: BBC na mitandao mingine mbalimbali ya kijamii

Written by simbadeo

March 6, 2013 at 12:15 pm