simbadeo2000

WAZA MPAKA BASI (THINK TO NO END).com weblog NOTE: Views or opinions expressed in this blog do NOT in any way represent those of any organisation, community, association, company, circle of friends, religious or ethnic group to which I am associated with.

Heri ya Sikukuu ya Idd el Fitr … Ujumbe wa Vatican katika Siku Hii

leave a comment »

Hii ni maalumu kwa ajili ya kuwatakia Ndugu Waislamu popote walipo duniani heri na baraka tele kwa sikukuu ya Idd el Fitr. Ama kwa hakika mmemaliza kipindi muhimu sana na bila shaka mmepata thawabu nyingi za kuwawezesha kuuishi mwaka huu mwingine hadi Ramadhan ijayo. Pichani ni msikiti uliojengwa mwaka 1969 kule Mpanda Ndogo wilayani Mpanda, Katavi.

Sambamba na salamu zangu hizo. Hapa chini ninawaletea salamu za Kanisa Katoliki kama zilivyotolewa na Vatican na pia kuchapishwa na Gazeti la Kiongozi la hapa nchini wiki iliyopita. Karibuni na kila la kheri.

Ujumbe wa Kanisa Katoliki wa Kumaliza Mwezi wa Ramadhani

Kuwaelimisha vijana kuhusu haki na amani

Kwa ajili ya kumaliza Ramadhani, kipindi ambacho Waislamu hufunga na kuabudu, katika Sikukuu ya Idi ya mwaka wa Kiislamu wa 1433 ambao ni 2011 Baada ya Kristo, Kardinali Jean-Loius Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Mazungumzo Baina ya Imani mbalimbali, na Askofu Mkuu Pier Luigi Celata, Katibu, walituma ujumbe katika lugha tofauti 31 kwa jumuiya za Waislamu zikiwa na ujumbe: “Kuwaelimisha vijana Wakristo na Waislamu masuala ya haki na amani”. Ujumbe huo ni huu hapa chini ambapo umetafsiriwa kutoka katika lugha ya Kiingereza.

Wapendwa marafiki Waislamu,

1. Mnaposherehekea Sikukuu ya Idi ambayo inaashiria mwisho wa mwezi wa Ramadhani, unatupa sisi tulio katika Baraza la Kipapa kwa ajili ya Mazungumzo ya Imani Tofauti furaha ya kuwapa salamu zetu za upendo kwenu.

Tunafurahi pamoja nanyi kwa ajili ya kujaaliwa wakati huu ambao unawapa ninyi fursa ya kukuza zaidi utii wenu kwa Mungu, kwa kufunga na kutenda matendo mengine mema, jambo ambalo hata kwetu ni la thamani kubwa.

Ni kwa sababu hii kwamba mwaka huu, tuliona ni vema tulenge katika tafakari ya pamoja kuhusu elimu kwa vijana wa Kikristo na Waislamu kwa ajii ya haki na amani, mambo mawili ambayo hayawezi kutenganishwa na ukweli na uhuru.

2. Kama jukumu la elimu limekabidhiwa kwa jamii nzima, kama mnavyojua, basi kwanza kabisa, na kwa namna ya pekee, ni kazi ya wazazi na, pamoja nao, familia, shule, vyuo vikuu na pasipo kusahau wajibu wa wale wanaohusika na dini, utamaduni, jamii na maisha ya kiuchumi, na ulimwengu mzima wa mawasiliano.

Ni harakati ambayo ni nzuri na ngumu: kuwasaidia watoto na vijana kugundua na kuendeleza zawadi za asili ambazo Muumba alitujaalia na kujenga uhusiano wa kinadamu unaoenda na wajibu. Kwa kurejea kwenye wajibu wa waelimishaji, Baba Mtakatifu Benedikto XVI hivi karibuni alithibitisha: “Kwa sababu hii, katika siku hizi kuliko ilivyopata kuwa hapo kabla tunahitaji mashahidi wa kweli, na siyo tu watu ambao kazi yao ni kutunga sheria na kueleza ukweli wa mambo … Shahidi ni mtu ambaye kwanza anaishi maisha ambayo anawataka wengine waishi. (Ujumbe uliotolewa katika Siku ya Amani Duniani” 2012).

Zaidi ya hilo, hebu tukumbuke kwamba vijana nao wana wajibu vile vile kwa elimu yao na kwa makuzi yao kuhusiana na haki na amani.

3. Haki huainishwa kwanza kabisa na utambulisho wa binadamu, katika ujumla wake wote; haiwezi kuchukuliwa tu katika maana zake za matokeo yale yale na mgawanyo fulani. Tusisahau kwamba maendeleo kwa wote hayawezi kupatikana pasipo mshikamano na upendo wa kidugu!

Kwa wanaoamini, haki ya kweli, inapozingatiwa kupitia urafiki na Mungu, husaidia kukuza uhusiano mwingine wowote uliopo: kwa nafsi ya mtu mwenyewe, kwa watu wengine na kwa ulimwengu mzima.

Zaidi ya hayo, hao wanaoamini hukiri kwamba haki ina asili yake katika ukweli kwamba binadamu wote wameumbwa na Mungu na wote wanaitwa ili wawe kitu kimoja, familia moja. Mtazamo huo, huku fikra na uwazi vikipewa heshima inayostahili, unawahimiza watu wote waume kwa wake wenye mapenzi mema, ukiwaalika kuleta uhusiano uliotengemaa wa haki na wajibu.

4. Katika ulimwengu wetu uliojaa mahangaiko, kuwaelimisha vijana kuhusu amani ni jambo linalozidi kuhitaji haraka ya aina yake. Ili kujishughulisha na hili kwa kiwango cha kutosha, hapana budi kuielewa ipasavyo asili ya kweli ya amani: kwamba kuwepo kwa amani hakuna maana ya kutokuwepo vita tu, au kuwepo kwa uwiano kati ya pande mbili hasimu, bali ni wakati huo huo sawa na zawadi kutoka kwa Mungu na kivutio cha binadamu anachopaswa kukitafuta pasipo kuchoka.

Ni tunda la haki na matokeo ya hisani. Ni muhimu kwamba waumini waendelee kuwa watu wanaojishughulisha kikamilifu katika jamii zao: kwa kuishi huruma, mshikamano, ushirikiano na undugu, ili kwa ufanisi waweze kuchangia kushughulikia changamoto kubwa zinazoukabili ulimwengu wa leo: ukuaji uliotengemaa, maendeleo yaliyo shirikishi, kuzuia na kutafuta suluhu kwa migogoro, kwa kutaja machache tu.

5. Kwa kuhitimisha, tungependa kuwahimiza vijana Waislamu na Wakristo wanaosoma ujumbe huu kuendeleza ukweli na uhuru ili kuwa watangazaji wa kweli wa haki na amani na wajenzi wa utamaduni ambao unaheshimu utu na haki za kila raia. Tunawasihi wawe wavumilivu na wastahimilivu, mienendo ambayo ni muhimu katika kufikia matamanio haya, na pasipo kuangukia kwenye suluhu zenye mashaka, njia za mkato zilizo danganyifu au njia zisizoheshimu utu wa mtu.

Ni waume kwa wake wale tu waliojiaminisha kuhusu umuhimu na uzito wa masuala watakaoweza kujenga jamii ambapo haki na amani zitaonekana wazi wazi na kuwa sehemu ya maisha ya kila siku.
Mungu awajaalie mioyoni mwao unyenyekevu na matumaini, familia na jamii ambazo zinapigania nia ya kuwa ‘nyenzo za amani’!

Tunawakia Sikukuu njema nyote!
Kutoka Vatikani,
Tarehe 3 Agosti 2012

Advertisements

Written by simbadeo

August 18, 2012 at 8:25 pm

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: