simbadeo2000

WAZA MPAKA BASI (THINK TO NO END).com weblog NOTE: Views or opinions expressed in this blog do NOT in any way represent those of any organisation, community, association, company, circle of friends, religious or ethnic group to which I am associated with.

London … motoni

leave a comment »

Waziri Mkuu wa Uingereza, Bw David Cameron, akizungumzia matukio ya ghasia yaliyolikumba jiji la London kwa siku tatu mfululizo. Ameeleza kwamba yanayoendelea ni ‘unyama katika picha yake halisi’.

Moja ya majengo yakiteketea kule London, Uingereza.

Picha ya Press Association … moto ukitafuna jengo katika kitongoji cha Tottenham.

Ni mabaki ya basi lililoteketea kwa moto … Picha ya Press Association.

‘Basi la ghorofa’ nalo likiteketea kwa moto. Picha ya REX.

Je, nini chanzo cha ghasia kule London, Uingereza?

Ghasia zilianza baada ya kile kinachosadikiwa polisi kumwua kwa kumpiga risasi mtu aliyefahamika kama Mark Duggan Alhamis jioni. Kundi la watu wapatao 300 walijikusanya nje ya kituo cha polisi cha Tottenham wakidai ‘haki’ itendeke, ilikuwa usiku wa Jumamosi iliyopita. Vitendo vya uporaji na uchomaji moto majengo na mali nyingine vilianza usiku huo. Polisi walishindwa kudhibiti hali ya mambo. Vitendo hivyo viliendelea na kusambaa katika vitongoji na miji mingine ikiwemo Birmingham, Liverpool, Nottingham na Bristol. Kutokana na hali ya mambo huko London, Waziri Mkuu, Bw David Cameron aliyekuwa mapumzikoni nchini Italia alilazimika kukatisha mapumziko yake.

Baada ya kurejea Uingereza, Bw Cameron, aliitisha kikao cha dharura cha baraza la mawaziri na walikibatiza ‘Cobra Meeting’. Wakati huohuo, jumla ya askari polis 16,000 walitumwa kwenye mitaa ya jiji la London pamoja na miji mingine iliyokumbwa na ghasia. Likizo zote za askari zimefutwa mpaka hali itakapotengemaa.

Matukio haya yamepokewa kwa mshangao na mshtuko katika kona mbalimbali za ulimwengu. Pengine ghasia na maandamano si vitu vilivyoshangaza sana. Kikubwa ni vitendo vya uporaji na wizi wa waziwazi ambavyo vimekuwa vikifanywa na makundi ya watu walio kwenye ghasia hizo.

Uingereza ni miongoni mwa mataifa yenye uchumi ulioendelea sana. Kwa mantiki hiyo, ingetarajiwa kwamba watu wengi zaidi wawe na hali bora kiuchumi kiasi cha kutopata tamaa ya kuiba au kuharibu mali za wengine. Je, nini kimetokea kiasi cha raia wa huko Uingereza kujishushia hadhi ya utu wao kwa kiasi hicho? Pengine vitendo hivi ni dalili kwamba uchumi wa taifa hilo umejenga matabaka ya kiuchumi kiasi kwamba kuna watu wasionufaika na maendeleo yaliyopatikana. Watu hawa wamekuwa ni ‘bomu lililokuwa likitafuta kulipuka’, na sasa limepata mwanya wa kulipuka. Kwa hiyo, tunachokiona sasa ni ‘kazi ya mikono ya mwanadamu’. Hakuna mwingine wa kumlaumu bali taifa lenyewe kwa kuruhusu kuwepo kwa tofauti kubwa kupita kiasi za kimapato.

Tukumbuke pia kwamba taarifa zinazoendelea kutolewa mpaka sasa ni kwamba zana za kisasa za mawasiliano … Facebook, Twitter, simu za mkononi n.k. zimetumika sana katika kueneza hayo yaliyotokea.

Je, matukio haya yana maana gani kwetu sisi tulio katika mataifa yanayoendelea … mataifa yenye uchumi duni? Kadiri siku zinavyopita, ndivyo tunavyozidi kushuhudia watu wachache katika jamii wakijilimbikizia utajiri mkubwa kupita kiasi, mara nyingi kwa njia zisizo za haki, na wakati huohuo makundi makubwa ya watu, hasa vijana, wakiachwa kuishi maisha ya kubangaiza. Ukitembea katika majiji makubwa katika Afrika Mashariki, mathalani, si jambo la ajabu tena kuona vijana mamia kwa mamia, al maarufu kama machinga, wakichuuza biashara barabarani na kwenye makutano ya barabara; achilia mbali wale wanaotembea katika sehemu za starehe kama baa n.k. Vijana hawa ni ‘bomu linalotafuta kulipuka’ wakati wowote.

Siku bomu hilo litakapolipuka … tutashuhudia (ikiwa tutapata bahati ya kubaki hai) uharibifu mkubwa zaidi ya ule tunaoona ukitokea kule Uingereza. Kumbe basi nini kifanyike … hakuna majibu mepesi katika hili … kikubwa ni kuleta fursa nyingi za kazi ili watu wajipatie kipato ‘chenye hadhi ya kibinadamu’, watu waweze kumudu kujiendeshea maisha yao kutokana na vipato hivyo. Kurejesha uwiano wa kimapato katika jamii. Hili wimbi la kibepari lina matatizo yake … kama tunavyoyashuhudia kule Uingereza. Na, tusipuuzie nguvu ya watu hawa tunaowachukulia kuwa ‘wa kawaida’, wanapogeuka … hakuna anayeweza kuwazuia. Tumeshuhudia nguvu ya ‘mitandao ya kijamii’ katika kuhamasishana kufanya jambo. Tuliona kule Tunisia, ikafuatia Misri, nchi mbalimbali za Kiarabu, tumeona kwa jirani zetu Malawi … Tusifikiri kwamba jambo hilo haliwezi kutokea kwetu … Afrika ya Mashariki. Ni wakati sasa watawala wajifunze kutokana na haya.

Tuendelee kutege sikio … siyo kwa ajili ya kufurahia Wazungu ‘wanavyoibiana’ bali kwa ajili ya kujifunza na kuona tujifunze nini ili kuzuia matukio ya aina hiyo huku kwetu. Nawakilisha.

Advertisements

Written by simbadeo

August 9, 2011 at 10:42 pm

Posted in Siasa na jamii

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: