simbadeo2000

WAZA MPAKA BASI (THINK TO NO END).com weblog NOTE: Views or opinions expressed in this blog do NOT in any way represent those of any organisation, community, association, company, circle of friends, religious or ethnic group to which I am associated with.

Philip Mangula aishauri CCM …

leave a comment »

Mzee Philip Mangula ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)

Mangula: CCM kujivua gamba hakutoshi

ATAKA WARUDI KWA MWALIMU NYERERE

Tumaini Msowoya, Iringa KATIBU Mkuu Mstaafu wa CCM, Phillip Mangula, amesema mabadiliko makubwa yaliyotokea ndani ya chama hicho, hayatoshi kukiimarisha na kusisitiza kuwa kuna umuhimu wa kukumbuka mfumo wa hayati Mwalimu Julius Nyerere wa kuwaenzi mabalozi wa nyumba kumi.Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi Jumapili kijijini kwake Imalinyi, Njombe, Mangula alisema mabalozi wa nyumba kumi wana uwezo mkubwa wa kukisimamia chama hicho na kwamba, bila kurejea mfumo huo mabadiliko yaliyofanyika hayatazaa matunda.

“Mabadiliko haya nimeyafurahia na lazima yawepo wakati huu tunapojiandaa na uchaguzi mwingine. Lakini pia tukumbuke kuwaenzi hawa mabalozi wa nyumba kumi ambao Nyerere aliwatumia kukijenga chama,” alisena na kuongeza:

“Wakati ule, kila mwanzo wa mwezi, tulikuwa tunafanya vikao ambavyo wanachama walikuwa wakiibua mijadala iliyokuwa inafanyiwa kazi.”

Mangula ambaye aliiongoza CCM kwa miaka kumi akiwa Katibu Mkuu (1996 hadi 2006), alisisitiza kuwa sehemu muhimu ambayo chama kinaweza kujengwa ni mashina kwa kuwatumia mabalozi wa nyumba kumi.

“Vikao vya wanachama vikirejeshwa nchi nzima, vinaweza kuleta matumaini makubwa ambayo yakiunganishwa na kujivua gamba, hali ya chama ya mwaka 2005, inaweza kurejea haraka,” alisema.

Aprili 10, mwaka huu wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Sekretarieti ya chama hicho walijiuzulu ikiwa ni mwanzo wa mageuzi makubwa ndani ya CCM.

Chiligati alisema lengo la mageuzi hayo ni kukijenga upya chama na kukiimarisha katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.

Wajumbe wa Sekretarieti waliojiuzulu, ni Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba manaibu makatibu wakuu wa CCM Bara, George Mkuchika na Visiwani, Saleh Ramadhan Feruzi na Katibu wa Itikadi na Uenezi, John Chiligati.Wengine ni Katibu wa Uchumi na Fedha, Amos Makala, Katibu wa Mipango, Kidawa Saleh na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mambo ya Nje, Bernard Membe.

Kwa mujibu wa Mangula, kama ngazi ya ubalozi, itasahauliwa na kukumbukwa wakati wa chaguzi ambapo ajenda kuu huwa ni ushindi, hali inaweza kuwa tete zaidi kwa sababu wanachama watakuwa wamekata tamaa.

Alisema CCM inapaswa kutafakari mabadiliko yaliyokikumba kutokana na matokeo ya uchaguzi mkuu na kuhakikisha kuwa kinajipanga vizuri kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015.

“Najua uchambuzi wa hali na mazingira ndio umesababisha mabadiliko. Ilikuwa lazima tujihoji iweje chama kishuke kutoka asilimia 80.2 ya mwaka 2005 hadi asilimia 61.1 mwaka jana. Ni lazima Sekretarieti ya chama ijipange sawasawa kwa sababu hiyo ndiyo ubongo wa chama,” alisisitiza Mangula.

Kuhusu muswada wa Katiba mpya, Mangula alisema ni kweli kwamba hali ya sasa inahitaji katiba ambayo italingana na hali halisi na hiyo lazima ijadiliwe na wananchi wenyewe.

“Huku vijijini hatujaona mjadala unaohusu katiba zaidi ya kusikia kwenye redio. Ukimuuliza mwenyekiti wa kijiji na serikali yake kuhusu katiba iliyopo wala huo muswada unasema nini, hajui kwa sababu kelele nyingi zinasikika huko juu tu,” alisema.

Mangula ambaye amewahi kutumia nyadhifa mbalimbali katika Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Nyerere, alifahamisha mabadiliko ya Katiba ya miaka ya nyuma yalitokana na hali iliyokuwapo wakati huo, ingawa Watanzania wengi hawakuwa wanaijua.

Alisema lazima viongozi wa serikali za vijiji na wananchi vijijini wapewe elimu ya uraia ili waielewe katiba iliyopo na wapewe fursa ya kuijadili.

Mangula alikosoa kitendo cha muswada huo kuandikwa kwa lugha ya Kiingereza akisema anaamini kuwa haukulenga kumfikia mkulima, bali wasomi na watu wengine wa nje ya nchi wanaojua lugha hiyo.

CCM bado njia panda

Wakati huohuo, Fidelis Butahe na Exuper Kachenje wanaripoti kuwa, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ana wakati mgumu kusimamia utekelezaji wa uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya chama hicho kuwaondoa kwenye chama watuhumiwa ufisadi, baada ya kuibuka kundi la makada wa chama hicho wanaowatetea watuhumiwa hao.

Wakati Nec ikiamini kuwa kuwaondoa watuhumiwa hao kutasaidia kukisafisha chama hicho, kundi hilo linaona hatua hiyo kuwa ni unafiki.

Kundi hilo linadai kuwa kama Nec inaona ni busara kuwaondoa watuhumiwa hao kwenye chama, basi viongozi wote walioingia madarakani kwa fedha chafu za EPA, waondoke.

Hata hivyo, tayari Sekretarieti mpya ya CCM imegundua mbinu hiyo ya kukwamisha utekelezaji wa agizo hilo la Nec na kutoa onyo kali kwa kundi hilo.

Wiki iliyopita Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nnauye, alisema Sekretarieti ya CCM, imebaini mbinu chafu zinazotumiwa na watuhumiwa hao wa ufisadi, kumchafua Rais Kikwete na familia yake kwa kutumia magazeti na vyama vya siasa na kuonya kuwa mbinu hiyo haitawasaidia, kwa sababu ni lazima watuhumiwa hao waondoke kwenye chama kama ilivyoagizwa na Kamati Kuu ya CCM na Nec.

Hata hivyo jana Nape, alipotakiwa kuzungumzia hali hiyo alisema anashangazwa na watu hao aliosema ni wachache wasiofikia kumi, kuzungumzia masuala hayo wakati si wajumbe wa Nec, wala Kamati Kuu.

“Bahati nzuri, hawajui maamuzi ya vikao vya Nec wala utekelezaji wake kwa sababu hawakuwemo ndani ya vikao na wala si wajumbe wa vikao vile. Kinachonishangaza zaidi wanayaita maoni ya wengi wakati watu wanaotoa hawafiki kumi,” alisema Nnauye.

Alisema anachokiona yeye kwa watu hao wachache, ni kama wametumwa kumtetea mtu fulani kwa umaarufu wake, akieleza kuwa ndani ya CCM maarufu ni chama na siyo mtu.

Aliongeza kuwa wanayosema watu hao ni maoni na mawazo yao binafsi ambayo kimsingi hawazuiwi kuzungumza, lakini akasema ikiwa wanataka yapokelewe ndani ya chama wayawasilishe kwa maandishi kupitia vikao vya chama, yatajadiliwa na yakikubalika yatafanyiwa kazi.

“Hayo ni mawazo yao, sioni kama wamefanya dhambi kuyatoa, ila wayafikishe katika vikao halali vya chama. Walete kwa maandishi yatasikilizwa, yakikubaliwa yatafanyiwa kazi, wakitoa maneno barabarani tutayaacha barabarani,” alisema na kuongeza:
“Tunayofanya, tunayoyasema tumekubaliana katika vikao, wao waseme nani kawaambia tunayofanya si maamuzi ya chama, wanapata wapi?”

Kuhusu kuwakabidhi barua watuhumiwa wa ufisadi, Nape alisema chama kilifanya maamuzi tofauti zaidi ya 27 na kwamba yote yanapitia hatua mbalimbali kabla barua kufikishwa kwa wahusika.
Hata hivyo, alisema hana hakika iwapo watuhumiwa wa ufisadi ndani ya CCM wameshakabidhiwa barua hizo.

“Tupo katika mambo ya Sikukuu ya Pasaka, sina hakika kama zimeshawafikia, lakini baada ya sikukuu nitakuwa ofisini hasa Jumatano, nitauliza na kujua kama wamefikishiwa barua hizo,” alisema Nnauye.

Mmoja wa makada wanaopinga kuondolewa kwa watuhumiwa hao wa ufisadi ni Balozi Paul Ndobho ambaye alikaririwa hivi karibuni akieleza kuwa kama kweli CCM inataka kujivua gamba, viongozi wote waliochaguliwa kwa kutumia fedha zilizoibwa kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), waanze wao kuondoka.

Alisema inashangaza viongozi wa CCM wanawaonyeshea vidole baadhi ya wanachama wake kuwa ndio vinara wa rushwa wakati wao wenyewe walipatikana kwa njia ya rushwa. Kada mwingine wa CCM anayepingana na uamuzi huo wa Nec ni Mkuu wa Mkoa Mstaafu, Stephen Mashishanga.

Pamoja na kupongeza mabadiliko kwenye Sekretarieti ya CCM, Mashishanga amepinga harakati za kuwaandama wanachama watatu kuwa ndiyo mafisadi.Alisema kuwashambulia makada hao wachache, hakuwezi kuisaidia CCM kurejesha umaarufu wake na kupendwa na wananchi.

Mashishanga alieleza moja ya mambo yaliyoipunguzia CCM kura katika uchaguzi uliopita kuwa ni wapinzani kuja na sera mbadala.David Msuya ni kada mwingine wa CCM aliyeibuka na kusema yuko tayari kuwatetea popote watuhumiwa hao wa ufisadi kwamba si mafisadi.

“Mimi nitaendelea kuwatetea kwa nguvu zangu zote kwamba si mafisadi na CCM na Serikali kama wanaweza kuthibitisha ufisadi wao, waende mahakamani,” alisema Msuya juzi mkoani Morogoro.

Kwa mujibu wa Msuya, kitendo cha Sekretarieti mpya ya CCM kuendelea kuzunguka nchini na kuzungumzia ufisadi bila kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watuhumiwa, ni kuwachafua.

Msuya ambaye pia ni mwanasheria anayeshughulikia haki za watoto, alidai kuwa baada ya mkutano wa kamati kuu na halmashauri kuu ya chama hicho kufanyika mkoani Dodoma ,chama hicho kiliibuka na msemo mpya wa kujivua gamba ambao kama hautatumika vizuri, huenda ukaendelea kukigawa chama hicho.

Tuhuma za ufisadi ndani ya CCM hazikuishia kuwataka watuhumiwa wajitoe kwenye chama pekee, bali zimeingia hadi kwenye Jumuiya yake ya Umoja wa Vijana (UVCCM).

Kada wa CCM na mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama hicho, Augustino Matefu amewataka viongozi wote wa UVCCM……….. akidai kuwa wamewekwa madarakani na mafisadi.
Kada huyo aliyezungumza na waandishi wa habari juzi aliushutumu uongozi huo kuwa uko kwa ajili ya kuwatumikia mafisadi watatu ambao wako katika mbio za kutafuta urais kwa mwaka 2015.

Matefu alimtaja kiongozi mwingine wa UVCCM kutoka Kanda ya Kaskazini kuwa naye anatumikia vibaya umoja huo na kuwashukia Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM, Beno Malisa na Katibu Mkuu, Martin Shigela kuwa wameshindwa kuwasaidia vijana walalahoi.

Uamuzi wa CCM kujivua gamba ulitokana na kauli ya Rais Kikwete Februari 5 mwaka huu wakati wa kilele cha chama hicho kutimiza miaka 34, baada ya kueleza kuwa chama hicho kilikuwa kimekosa mvuto kwa wananchi.

Habari ni kutoka Mwananchi Jumapili: Sunday, 24 April 2011 08:28

Photo credit: http://www.google.co.tz/imgres?imgurl=http://2.bp.blogspot.com/_Souln7A6cDQ/Rylt49iDgXI/AAAAAAAACao/_kr9cRsOhzk/s400/Mangula.jpg&imgrefurl=http://watanzaniaoslo.blogspot.com/2007_10_04_archive.html&h=400&w=343&sz=42&tbnid=F12JkOZ3JmJf2M:&tbnh=242&tbnw=208&prev=/search%3Fq%3Dphilip%2Bmangula%2Bphotos%26tbm%3Disch%26tbo%3Du&zoom=1&q=philip+mangula+photos&hl=en&usg=__wdS614FiYB-MYew2ImuXQITF9QI=&sa=X&ei=8wa0TeniFYjQhAeW5aDkDw&ved=0CBoQ9QEwAQ

Advertisements

Written by simbadeo

April 24, 2011 at 2:45 pm

Posted in Siasa na jamii

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: