simbadeo2000

WAZA MPAKA BASI (THINK TO NO END).com weblog NOTE: Views or opinions expressed in this blog do NOT in any way represent those of any organisation, community, association, company, circle of friends, religious or ethnic group to which I am associated with.

Sitta anusurika … ni katika hekaheka za rasimu ya muswada wa katiba mpya …

leave a comment »

Mh. Samuel J. Sitta (Picha kutoka vyanzo mbalimbali vya mtandao wa Intaneti)

Sitta anusurika kipigo
• Aondolewa na FFU ukumbini

na Mwandishi wetu, Dodoma

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais (Muungano) Samia Suluhu Hassan, wamenusurika kipigo baada ya kutokea vurugu kwenye kikao cha kujadili muswada wa mabadiliko ya Katiba mpya visiwani Zanzibar.

Sitta, alikuwa akiwasilisha rasimu ya marejeo ya katiba kwa niaba ya Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani, ambapo wakati akitoa mada hiyo hali ndani ya ukumbi ilikuwa shwari.

Vurugu hizo zilitokea katika ukumbi wa Shule ya Haile Selassie mjini Zanzibar jana, baada ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed, kuchangia kwa maneno makali na baadaye kuuchana hadharani muswada huo na kutoka nje ya ukumbi.

Tukio hilo lilisababisha baadhi ya wajumbe kuzichana nakala za muswada huo huku wengine wakinyanyua viti juu wakiashiria kwamba mkutano huo umekwisha na baadhi yao wakimfuata Sheikh Farid nje ya ukumbi wa mkutano.

Kitendo hicho kilisababisha hali ya wasi wasi na kusababisha mtoa mada, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, kuondolewa kwenye ukumbi chini ya ulinzi mkali wa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).

Akichangia muswada huo, Sheikh Farid, alisema kabla ya kupelekwa muswada huo visiwani Zanzibar upelekwe wa Katiba ya Tanganyika, ili kuuangalia Muungano ambao hivi sasa haupo kwenye hali nzuri.

Alisema haoni sababu ya kujadiliwa mabadiliko hayo ya katiba kabla ya wananchi wa Zanzibar hawajaulizwa kwa njia ya kura ya maoni iwapo Muungano huo wanautaka au hawautaki.

“Napenda kutoa usia wangu kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya umoja wa kitaifa kuitisha kura ya maoni wananchi waulizwe wanaotaka Muungano na wale wasioutaka”, alisema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maimamu, huku baadhi ya wajumbe wakinyanyua mabango yaliyoandikwa ‘Hatuutaki Muungano Jamani’.

Sheikh Farid, alisema zama za udikteta wa Nyerere zimekwisha, wananchi wa Zanzibar wapo huru kutoa maoni yao na kama serikali inaogopa wananchi wapo tayari.

Naye aliyekuwa Katibu wa Umoja wa Vijana wa Afro Shirazy Party, Baraka Shamte, alisema muswada huo usijadiliwe hadi hapo marekebisho yatakapofanywa na kuundwa jopo la wanasheria kutoka pande zote mbili za Muungano.

Alisema muswada huo uandaliwe upya na yale yanayokosolewa yaondolewe kwa lengo la kufanikisha mpango wa kupata katiba itakayosaidia kuimarisha Muungano wenyewe.

Akichangia muswada huo, Diwani Arafa Mohammed Said, alisema kuna haja ziundwe tume mbili za kukusanya maoni juu ya Katiba mpya, ikiwemo tume ya Tanzania Bara na tume ya Zanzibar .

Alisema kwakuwa Zanzibar wananchi wake ni wachache si vizuri wakaingizwa katika mjadala wa jumla na hatua hiyo ya kuundwa tume mbili itawapa nafasi ya kupata ukweli juu ya kile wananchi wa Zanzibar wanachokitaka.

Mwanasheria, Abdulkadir Mohammed Amour, alisema bila ya marekebisho yanayopigiwa kelele kufanyika, muswada huo iwapo utapitishwa na Bunge mwisho wake utakuwa Kisiwa cha Chumbe na hautahusu Zanzibar.

Askari mstaafu, Miraji Kiongwe, alisema inashangaza tangu kufikiwa Muungano wa mwaka 1964, vyombo vya ulinzi na usalama vimekuwa vikiongozwa na wakuu wake kutoka upande mmoja wa Muungano.

Alisema hakuna mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) au Jeshi la Polisi hata mmoja aliyetoka Zanzibar, wakati vyombo hivyo ni vya Muungano.

Akitaja majina ya wakuu waliowahi kuongoza vyombo hivyo, alisema vyombo hivyo havina tofauti na Bunge, kwa vile hakuna spika hata mmoja aliyewahi kuongoza Bunge hilo kutoka Zanzibar.

Mwakilishi kutoka Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) Ibrahim Mzee, ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Wawakilishi, (BLW) alisema inashangaza tume zote zilizowahi kuundwa Zanzibar imekuwa ikipewa nafasi ya umakamu na mwenyekiti hutoka upande wa Tanzania Bara.

Alitoa mfano wa tume hizo kuwa ni ile ya Jaji Kisanga, Jaji Nyalali na kutaka utaratibu huo kuangaliwa upya, ili Zanzibar nayo iweze kutoka watu wa kuongoza tume hizo za kitaifa.

Akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo, alisema Bunge la Muungano halina mamlaka ya kutunga katiba na kazi hiyo inatakiwa kufanywa na Bunge la Katiba.

Alisema kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano kazi yake ni kutunga sheria, hivyo kuwepo na Bunge la Katiba na lazima liwe na wajumbe sawa kutoka Zanzibar na Tanzania Bara.

Alieleza kwamba muswada huo una upungufu mwingi na kushauri kuwa unahitaji kuangaliwa upya, ikiwamo mamlaka makubwa aliyopewa Rais wa Jmahuri ya Muungano.

Mzee alisema haikuwa muafaka kusema wajumbe wa tume hiyo uteuzi wao ufanyike kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar, kwa vile suala la ushauri ni jambo la hiari na badala yake kuwepo makubaliano kati ya viongozi hao.

Akizungumzia vurugu hizo, Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan, alisema waliofanya vurugu hizo ni wahuni.

Alisema kikundi hicho cha wahuni kilikwenda katika mkutano huo kwa malengo maalumu, ili ionekane watu hawataki Muungano.

Aidha, alisema amesikitishwa na kitendo cha watu kuchana nakala za muswada huo na kutoa wito kwa wananchi kujiepusha na vitendo vya jazba, lakini alisema maoni yote yaliyotolewa kamati imeyachukua na itayafanyia kazi.

Wakati huo huo, Chama cha Wanasheria wa Tanzania Bara (TLS), wameukosoa Muswada wa Marejeo ya Katiba unaotarajiwa kuwasilishwa katika kikao cha Bunge kinachoendelea mjini Dodoma kutokana na kuwa na kasoro nyingi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Rais wa TLS Francis Tola, alisema wanatarajia kukutana na Rais Kikwete ili kumshauri juu ya mapitio ya muswada huo.

“Muswada ni mzuri (kwa wazo), lakini una kasoro nyingi, haustahili kupelekwa bungeni na kupitishwa bali wananchi wapewe muda wa kutosha ili kutoa maoni yao kwanza,” alisema.

Alisema muswada huo umepelekwa bungeni kwa mfumo wa hati ya dharula, hivyo ni kama kitendo cha zima moto kinafanywa na serikali ili kupata maoni ya wananchi na wadau mbalimbali kwa muda mfupi.

Rais wa TLS alisema hati ya dharura pia inawanyima uhuru na haki kwa wananchi na wadau mbalimbali wa sheria kushiriki katika kutoa maoni yao kwa muda mrefu.

Alisema kitendo cha kuandaa mijadala ya wazi ya Muswada wa Marejeo ya Katiba kwa mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar kwa niaba ya wananchi wa mikoa mingine si haki na usawa.

“Naona serikali inafanya haraka katika jambo hili, na wanachukulia mzaha, haiwezekani ukafanya mijadala katika mikoa hiyo na kuafiki kwamba hayo yaliyotolewa ndiyo mapendekezo ya wananchi wote wa Tanzania.

Tunamtaka Rais Kikwete na Mwanasheria Mkuu kuondoa hati ya dharula, endapo hawatatekeleza pendekezo hilo ni wazi kwamba hakutakuwa na maana nzima ya kupata maoni kutoka kwa wananchi na wadau wengine,” alisema.

Aliongeza kuwa muswada huo una kasoro ya lugha, kutokana na kuandikwa kwa lugha ya Kiingereza, hali itakayowafanya wananchi wasiofahamu lugha hiyo kutoshiriki kikamilifu katika kutoa maoni.

Alitaja kasoro nyingine ni kupewa jina la Muswada wa Mapitio ya Katiba, lakini unajipinga wenyewe kutokana na kuwa na kifungu kinachoeleza kwamba muswada huo ni wa Kutunga Katiba Mpya.

Alisema kuundwe Bunge la Katiba litakalowajumuisha wadau mbalimbali ambalo litakuwa na jukumu la kuratibu masuala ya Katiba.

Chanzo cha habari: Tanzania Daima Jumapili 10 Aprili 2011
*********

Tafakari fupi

Habari hiyo inaashiria kwamba mambo si shwari hata kidogo. Hatuna budi kama Taifa kutumia njia sahihi na isiyo na mizozo ya kuleta Katiba mpya. Tunapolazimisha matumizi ya njia ambazo zinaashiria kuwa na ‘ujanjaujanja’ … basi tuelewe kwamba tunaliweka Taifa mahali pabaya. Mungu atujalie hekima na busara ya kuona namna ya kutenda haki huku tukizingatia maslahi na mustakabali mwema wa Taifa hili. Amen.

Advertisements

Written by simbadeo

April 10, 2011 at 1:35 pm

Posted in Siasa na jamii

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: