simbadeo2000

WAZA MPAKA BASI (THINK TO NO END).com weblog NOTE: Views or opinions expressed in this blog do NOT in any way represent those of any organisation, community, association, company, circle of friends, religious or ethnic group to which I am associated with.

Hotuba ya Mh Rais JK … na upepo unaovuma ulimwenguni

leave a comment »

Baada ya muda kutakuwa na kuchorwa upya kwa mipaka ya nchi za Afrika hasa baada ya Sudani ya Kusini kupiga kura ili ijitenge kutoka iliyokuwa Sudani. Upepo wa mageuzi unaoendelea kuvuma katika nchi mbalimbali huenda pia ukaathiri mipaka ya baadhi ya nchi. Mgogoro wa kisiasa uliopo nchini Ivory Coast nao huenda utakuwa na nafasi katika uchorwaji upya wa mipaka ya Afrika. Hata hivyo, bado ni mapema kusema kwa uhakika.

Dk. Slaa: Moto ni ule ule

• KIKWETE ASAFIRI TENA NJE, CUF NAO WAMSHAMBULIA

na Waandishi wetu

WAKATI Rais Jakaya Kikwete akihamishia matatizo yanayolikabili taifa katika mikono ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwamba wanachochea vurugu, viongozi wa chama hicho wamejibu mapigo kwa kumtaka aache kuogopa kivuli chake na kama ameshindwa kuliongoza taifa, ajiuzulu mara moja.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa chama hicho taifa, Dk. Wilbrod Slaa, wakati wa mahojiano na gazeti hili jana.

Dk. Slaa na viongozi wenzake, akiwemo mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe, ambao wako mikoa ya Kanda ya Ziwa wakifanya mikutano ya hadhara maarufu kama Operesheni Sangara, alisema wameshangazwa na kauli ya Rais Kikwete kwamba CHADEMA inafanya vurugu ili kuvunja amani ya nchi.

“Tunataka kumwambia Rais Kikwete kuwa hakuna Mtanzania mwenye hofu na CHADEMA, isipokuwa ni hofu na ‘msoto’ wa maisha magumu na ya mateso bila chuki! CHADEMA si tishio kwa usalama wa nchi bali ni kielelezo cha utashi wa jamii ya walalahoi na wavuja jasho maskini wenye shida, dhiki na taabu za maisha ya kiuchumi, kijamii na kisiasa,” alisema Dk. Slaa.

Dk. Slaa ambaye amepata kuwa mgombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita na kutoa upinzani mkubwa kwa CCM, aliendelea kusema Rais Kikwete ni kiongozi aliyeshindwa kuleta maisha bora, sasa amefikia hali ya woga na ana wasiwasi na hali tete ya wananchi kwani ameshachoka akili na hawezi tena kufikiria utatuzi wa matatizo ya wananchi wake.

“Ukweli ni kwamba Watanzania wana kero za maisha magumu na hawahofii usalama wa maisha yao mikononi mwa CHADEMA. Na yeyote anayesema juu ya CHADEMA kuvuruga amani ya nchi ni katika kujenga hoja nyepesi ili kwa hoja hiyo chakavu CHADEMA kama chama kionekane mbele ya macho ya jamii kwamba ni chama cha vurugu,” alisema kiongozi huyo maarufu nchini.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa, Rais Kikwete ana wajibu wa kurekebisha hali ya uongozi wake ili kuleta tija na ufanisi kiuchumi na kijamii kwani Watanzania wanataka hali bora na si maneno yasiyokuwa na mashiko.

“Kikwete anapaswa kujua kwamba ukiona wananchi wamechoka na kupigika kimaisha, usiwahubirie amani na utulivu kwa kuwa hakuna amani mahala penye shida, dhiki, taabu ya maisha na njaa,” alisema.

Aliwaahidi Watanzania kuwa CHADEMA imejipanga kufanya mikutano nchi nzima kuelezea matatizo yanayolikabili taifa kwa sasa na kusisitiza CHADEMA haina uwezo wa kumng’oa Rais madarakani bali wananchi ndiyo wenye uwezo huo wakiamua.

Akizungumzia kauli hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, Profesa Mwesiga Baregu, amemshangaa Rais Kikwete na kumwita kuwa mwoga wa siasa za upinzani na kumtaka awe na ngozi ngumu.

Baregu alisema hakutegemea kama Rais angetumia muda mwingi kuilaumu CHADEMA badala ya kuzungumzia matatizo yanayoikumba taifa.

“Nimeshangaa kidogo nadhani Rais sio mkomavu wa upinzani, ni kama vile anataka kulishtua taifa bila kuwa na sababu; CHADEMA inazungumza mambo ya kawaida kabisa katika mikutano yake huko ni kutokomaa na siasa na woga usio na sababu,” alisema Prof Baregu.

Alisema kama CHADEMA wamekuwa wakifanya mikutano yao na kuifananisha nchi kuweza kuwa kama Libya ni kutokana na kuwa na matatizo mengi ambayo hayajapatiwa ufumbuzi hivyo aliitahadharisha serikali ya CCM kuwa makini.

“Sisi tunafanya kazi za kuwaambia watu CCM ndio iliyotufikisha hapa tulipo hatuna makosa na wanatakiwa kufanya mambo ya msingi ambayo Watanzania wanayahitaji na kama hawajafanya kuna hatari ya kutokea ya Libya, tatizo liko wapi?” alihoji Profesa huyo.

CCM yapigwa ganzi

Wakati Rais Kikwete akiamua kuwalipua viongozi wa CHADEMA, ndani ya chama hicho viongozi wake ni kama wamepigwa ganzi kiasi cha kushindwa kuamua jinsi ya kujibu hoja zinazotolewa na viongozi wa CHADEMA kwenye mikutano yao ya hadhara ya Operesheni Sangara.

Baadhi ya vigogo wa CCM waliozungumza na gazeti hili, walisema kuwa chama hicho kimegawanyika kuhusu mbinu itakazozitumia kujibu hoja za CHADEMA kwani baadhi wanataka uitishwe mkutano wa vyombo vya habari, huku wengine wakipendekeza waende kwenye mikutano ya hadhara katika maeneo waliyopita CHADEMA.

“Tatazo tulilonalo sasa, nani atasimama kwenye mikutano ya hadhara kuhutubia kupinga hoja za CHADEMA na watu wakamsikiliza? Je, tukienda mikoani walimopita CHADEMA, nasi tutapata idadi kama ile ya CHADEMA? Lakini tukiamua kuitisha mkutano wa wana habari, utakuwa na maana kama ile mikutano ya hadhara ya Operesheni Sangara?” alihoji mmoja wa viongozi wa CCM.

Kigogo huyo ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) na Mkutano Mkuu wa chama hicho tawala, alikiri kuwa CHADEMA imekiweka chama hicho katika wakati mgumu na hiyo imetokana na udhaifu wa CCM katika kushughulikia kero za wananchi.

“Hoja zote za CHADEMA, tumewapa wenyewe kwa sababu ya udhaifu wetu kiuongozi hasa tabia ya kupenda kulindana. Angalia matatizo kama ya mgawo wa umeme na kupanda kwa gharama zake, sakata la ufisadi wa Dowans na Richmond, wizi wa EPA, Kagoda, ukosefu wa ajira, makundi yanayokinzana ndani ya CCM, maisha magumu ni miongoni mwa mambo tuliyoyaachia na ndiyo CHADEMA wanayatumia kutushambulia, hapa uchochezi uko wapi,” alihoji kigogo huyo.

Hotuba yake yamponza

Wananchi mbalimbali waliotoa maoni yao wameishutumu hotuba ya Rais Kikwete wakisema kuwa ni ya uchochezi.

Mwenyekiti wa taasisi isiyo ya kiserikali ya FORD, Seneta Julius Miselya, alisema jana kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) si wachochezi kama anavyosema Rais Kikwete bali anayechochea hayo ni Rais mwenyewe kwa kushindwa kutimiza wajibu wake kwa wananchi.

“Hotuba yake ni ya uchochezi, napinga kwa nguvu zote kuwa CHADEMA ni wachochezi bali wanazungumza ukweli kwamba wakipata madaraka watawatendea vipi wananchi. Sisi hatuoni mantiki yoyote kuishutumu,” alisema Miselya.

Aliongeza kuwa Rais Kikwete ameshindwa kuwatimizia wananchi maisha bora hali ambayo inasababisha maisha ya sasa kuwa magumu mara tano ya wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa.

Alimshauri kujiuzulu kwani hali inayoendelea kutokea nchini ni matokeo mabaya ya utawala wake.

Aliitaka CHADEMA kutotishika na kauli ya Rais bali kuendeleza wimbi lao la kukutana na wananchi ili kuwaelimisha kuhusu mambo mbalimbali.

Naye Jerry Tillya alimshangaa Rais kwa hatua yake ya kutumia muda mwingi kuiponda CHADEMA badala ya kueleza matatizo yanayoikabili nchi.

Alisema hivi sasa nchi inakabiliwa na wimbi la mgawo wa umeme, maisha magumu lakini badala ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo ameigeuza hotuba yake kuwa uwanja wa kufanya kampeni.

Alisema badala ya kutoa shutuma angewaeleza wananchi katika kipindi cha siku 100 za uongozi wake ametekeleza jambo gani la maana.

Naye Amina Hassan, alisema Rais anapaswa kutumia busara hasa katika kuzungumzia vitu vinavyoigusa nchi.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Mtatiro Julius, alisema alichokifanya Rais katika hotuba yake ni kuwadanganya Watanzania kwani hali ya maisha kwa sasa inatisha.

Alitolea mfano tatizo la umeme nchini ambalo lilikuwepo tangu alipofariki Mwalimu Julius Nyerere ambalo halijapatiwa ufumbuzi hadi leo na hiyo inatokana na mikakati mibovu ya uongozi.

Kuhusu tatizo la njaa alisema hali hiyo inatokana na serikali kutokuwa na mipango madhubuti ya kuitokomeza kwa kuwawezesha wakulima bali inachokifanya ni kubadili maneno na misamiati ya kilimo kila kukicha.

Naye Juma Khalfan, alisema ameshangazwa na Kikwete kuzungumza masuala ya maandamano ya CHADEMA na jambo hilo linaonyesha dhahiri asivyojiamini.

“Tunazidi kupoteza imani na Rais wetu, wananchi tuna matatizo mengi yanayotukabili badala ya kutueleza namna ya kuyakabili tunashangaa kuona anatueleza masuala ya CHADEMA, hii inaonyesha kwamba hajiamini kabisa,” alisema Khalfan.

“Tulitegemea atatuahidi kumaliza matatizo hata kwa asilimia kidogo lakini anasema hawezi kuyamaliza kwa kuwa Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa hawakufanya hivyo.

“Yeye alitakiwa awaonyeshe mfano marais waliopita na sisi wananchi wake tuliomchagua kwa imani kubwa,” alisema Olotu.

Kikwete safarini tena

SIKU tano baada ya kurejea nchini akitokea nchini Mauritania na baadaye Ivory Coast, Rais Jakaya Kikwete ameondoka tena nchini jana kuelekea Paris, Ufaransa, kuhudhuria mkutano wa siku mbili wa kimataifa wa Tansnia ya Uzinduaji (Global Extractive Industries Transparency Initiative -EITI).

Katika mkutano huo unaoanza leo, Rais Kikwete anatarajiwa kutoa mada juu ya umuhimu wa shughuli za uziduaji na uwazi katika mapato ya madini.

Baada ya kumaliza mkutano huo wa Paris, Ufaransa, Rais Kikwete atasafiri kuelekea Noukchott, Mauritania kwa ajili ya kikao cha marais wa Afrika wanaotafuta suluhisho la tatizo la kisiasa nchini Ivory Coast.

Akiwa nchini Mauritania, Rais Kikwete atajiunga na marais wa Mauritania, Afrika Kusini, Burkina Faso, Chad, Nigeria na Equatorial Guinea pamoja na wawakilishi wa Jumuia ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU) Balozi Jean Ping na Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN).

Ivory Coast imegawanyika katika sehemu mbili, moja ikimuunga mkono aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo, Alassane Quattara, na nyingine ikimuunga mkono Rais aliyekuwa anatetea kiti chake katika uchaguzi huo, Laurent Gbagbo.

Chanzo: Tanzania Daima, Jumatano 2 Februari, 2011

Nyongeza:

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Jakaya Mrisho Kikwete, hivi sasa inatawala mazungumzo ya watu kwenye kila aina ya vijiwe mijini na vijijini. Ukiwa kwenye daladala, ukiwa kwenye vijiwe vya kahawa, ukienda kwenye viti virefu, ukiwa kwenye vikao vya kiti moto … ni hotuba ya Mheshimiwa Rais. Ni hotuba nzito na bila shaka Watanzania wanaendelea kuitafakari kwa kuzingatia maslahi ya Taifa ya sasa na ya baadaye. Ni wakati sasa washauri wa Mheshimiwa Rais nao wafanye kazi kwa bidii zaidi … hasa ya kusoma hali ya mambo nchini na kimataifa ili kutokana na ushauri wao, uongozi wa nchi uimarike katika kukabili changamoto tulizo nazo katika zama zetu hizi. Inawezekana kuvuka bahari hii iliyokosa utulivu pasipo kupoteza hata unywele mmoja wa mwenzetu. Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

Advertisements

Written by simbadeo

March 2, 2011 at 11:49 am

Posted in Siasa na jamii

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: