simbadeo2000

WAZA MPAKA BASI (THINK TO NO END).com weblog NOTE: Views or opinions expressed in this blog do NOT in any way represent those of any organisation, community, association, company, circle of friends, religious or ethnic group to which I am associated with.

Mnyika: Kwa nini mitambo ya Dowans isitaifishwe?

leave a comment »

Jengo la TANESCO Makao Makuu, Ubungo, Dar es Salaam …

Mnyika: Dowans wafute fidia ICC

• ASEMA HILO LITAEPUSHA MITAMBO YAO KUTAIFISHWA

na Mwandishi wetu

WAZIRI Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika (CHADEMA) amewataka wamiliki wa Kampuni ya kuzalisha umeme ya Dowans kujitokeza hadharani na kufuta fidia ya shilingi bilioni 94 ambazo wanatakiwa kulipwa na Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO).

Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo, alisema iwapo wamiliki hao wa Dowans wataweza kutekeleza pendekezo lake la kufuta fidia hiyo iliyoamriwa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICC) wanaweza kuiokoa mitambo yao ya kuzalisha umeme iliyopo Dar es Salaam kutotaifishwa.

Mbunge huyo kijana, alisema mbali ya kufuta kwa hiari yao fidia hiyo, wamiliki hao wa Dowans wanapaswa kukiri pia kwamba walirithi mkataba wenye utata wa Richmond kwa kupotoshwa na kampuni hiyo na vyombo vya serikali.

Alisema anaamini iwapo Dowans watafanya hivyo, basi wanaweza kujijengea uhalali wa kuingia mkataba mpya wa kuzalisha umeme na TANESCO.

“Kampuni ya Dowans kama inataka kuepusha kutaifishwa basi wamiliki wake popote pale walipo duniani wajitokeze hadharani wakiri kwamba walipotoshwa na Richmond pamoja na vyombo vya kiserikali wakati wa kuhamishwa mkataba ili wajijengee uhalali wa kufanya majadiliano, ikiwamo ya kufuta madai ya fidia inayotaka kutolewa kwa mujibu wa hukumu ya ICC,” alisema Mnyika katika taarifa yake ya maandishi kwa vyombo vya habari aliyoitoa jana.

Mnyika alilazimika kutoa taarifa hiyo ili kusahihisha habari zilizochapwa katika gazeti moja la kila siku jana (si Tanzania Daima), ambalo lilimkariri mbunge huyo akitaka Dowans ipewe mkataba wa miezi mitatu wa kuzalisha umeme ili kupunguza makali ya mgawo wa umeme.

“Sijawahi kutoa kauli popote ya kushauri Dowans ipewe mkataba wa miezi mitatu kama ilivyonukuliwa na chombo kimoja cha habari,” alisema Mnyika.

Mbunge huyo alisema katika kauli yake iliyonukuliwa kwa makosa kutokana na mahojiano aliyoyafanya juzi kupitia TBC, alisema aliitaka serikali itumie sheria hususan ya uhujumu uchumi kuiwasha mitambo husika (Dowans) kwa masilahi ya taifa.

“Ningependa kutumia fursa hii kusisitiza mtazamo wangu kwamba ni muhimu ili kupunguza adha ya mgawo wa umeme, serikali itumie mamlaka yaliyopo kwenye Katiba na sheria ikiwemo sheria ya uhujumu uchumi, sheria ya kupambana na rushwa, sheria ya mali zilizopatikana isivyo halali itaifishe mitambo hiyo haraka iwezekanavyo na kuiwasha kwa masilahi ya umma,” alisema Mnyika katika tamko lake la maandishi jana.

Akiendelea, Mnyika alisema kwamba Kampuni ya Dowans ilirithi mkataba kutoka Kampuni ya Richmond ambayo ilithibitishwa kwa maazimio ya Bunge kuwa ilipata mkataba katika mazingira ya ukiukwaji wa sheria, ikiwamo sheria ya kupambana na rushwa.

Mbali ya hilo, Mnyika alieleza pia kwamba hata kampuni yenyewe ya Dowans imeonekana kuwa na utata katika usajili, umiliki na uhamishaji wa mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura kutoka Richmond.

Mnyika alisema pia kwamba wananchi wanapaswa kutambua kuwa kiasi cha megawati 120 za Dowans hakiwezi kuziba pengo la takriban megawati 240 ambalo linalikabili taifa hivi sasa.

Alisema kwa sababu hiyo basi Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, anapaswa kutoa maelezo ya kina kuhusu hatua ambayo serikali inataka kuchukua ya kukodi mitambo ya MW 260.

“Waziri atoe ufafanuzi wa kutokukamilika kwa mipango ya serikali wakati ambapo dharura ya umeme ilijulikana tangu mwaka 2002, serikali ikaijadili kwa kina mwaka 2006, Bunge likapitisha maazimio mwaka 2008 na serikali ikaahidi tena mwaka 2009 kuweka utaratibu wa kukabiliana na dharura hiyo,” alieleza Mnyika, mmoja wa wabunge vijana makini katika kujenga hoja na kuchanganua mambo.

Mbunge huyo wa Ubungo alisisitiza haja ya Bunge kupatiwa fursa ya kujadili kwa kina suala la umeme katika mkutano unaoendelea wa Bunge kama jambo la dharura ili kuweza kulinusuru taifa.

Mnyika ambaye nia yake ya kutaka suala hilo la mgawo wa umeme lijadiliwe kwa dharura ndani ya Bunge juzi ilipingwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, akisema alikuwa akikusudia kutoa tamko lake rasmi wakati wowote.

“Nitatoa tamko la kina hivi karibuni kwa nafasi yangu ya uwaziri kivuli kuhusu suala la umeme, kwa kuzingatia hali ya mgawo inavyoendelea sanjari na kupanda kwa gharama za nishati hiyo kunakoongeza ugumu wa maisha kwa Watanzania walio wengi baada ya majadiliano na baraza kivuli na mamlaka nyingine husika,” alisema.

Chanzo: Tanzania Daima 17 Alhamis 2011

SWALI

Wadau hii imekaaje … naona kama ni njia nzuri ya kutupa nafuu katika sokomoko lililopo baina ya Dowans na Taifa letu … au siyo?

Advertisements

Written by simbadeo

February 18, 2011 at 4:00 pm

Posted in Siasa na jamii

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: