simbadeo2000

WAZA MPAKA BASI (THINK TO NO END).com weblog NOTE: Views or opinions expressed in this blog do NOT in any way represent those of any organisation, community, association, company, circle of friends, religious or ethnic group to which I am associated with.

Dowans …na … Nguvu ya Umma

leave a comment »

Simba wa Ngorongoro … Je, siku simba hao wakiamua kusiingilike kule Ngorongoro, nani atakayethubutu kufanya hivyo? Tukiwaheshimu kama ambavyo tumekuwa tukifanya … nao watatustahi … amani itaendelea kuwepo …

Dowans vita mpya

• NGUVU YA UMMA YAZIKABILI SHERIA ZA KIMATAIFA

na Mwandishi wetu

SAKATA la kampuni ya Dowans lililoibuliwa na maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) linazidi kuchukua sura mpya kila kukicha.

Katika hatua ya hivi karibuni, maamuzi hayo ya ICC ambayo yanalitaka Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kuilipa Dowans dola za Marekani milioni 65 (karibu shilingi bilioni 94) yamezidi kupingwa na makundi mbalimbali ya kijamii kwa namna na njia tofauti.

Matukio ya hivi karibuni yanayohusisha maandamano yaliyoandaliwa na vyama viwili vya upinzani, Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya kupinga Dowans kulipwa fidia hiyo ni ushahidi wa kwanza wa mapambano ya sheria za kimataifa na matakwa ya umma.

Mbali ya maandamano hayo ya CUF na CHADEMA, kauli za kuhoji au kupinga uamuzi huo wa ICC zilizotolewa na watu wenye majina makubwa, akiwamo Mama Maria Nyerere ambaye ni mjane wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ni kielelezo kingine cha mwenendo huo wa mambo.

Wakati mapambano dhidi ya malipo hayo yakiendeshwa nje ya wigo wa mahakama, vita nyingine dhidi ya maamuzi hayo ya ICC inaendelea katika Mahakama Kuu ambapo kundi la wanaharakati watetezi wa haki za binadamu limewakilisha pingamizi lao dhidi ya malipo hayo ya Dowans.

Habari kutokana na vyanzo vya kuaminika ndani ya serikali zinaeleza kwamba upinzani huo wa umma dhidi ya maamuzi ya ICC yanaiweka serikali njia panda na kushindwa kujua nini cha kufanya.

Kiongozi mmoja wa juu wa serikali aliye katikati ya sakata hilo, aliyezungumza na Tanzania Daima Jumatano kwa sharti la jina lake kutoandikwa gazetini alisema, kile kinachoonekana sasa kuwa ni hasira za wananchi dhidi ya Dowans kimejengwa katika misingi ya kuaminishwa kwao kwamba kampuni hiyo na ile ya Richmond ni hewa na zilishinda zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura wa megawati 100 katika misingi iliyokuwa na utata mkubwa.

Katika maelezo yake kwa gazeti hili, kiongozi huyo aliyekuwa akizungumza huku akiwa na hukumu ya ICC yenye kurasa 150 alisema serikali inapaswa kufanya kazi ngumu na kubwa kuuelimisha umma wa nini hasa kilitokea wakati wa hukumu hiyo iliyotolewa Novemba 15 mwaka jana.

“Kwa sasa tunaweza tukaendelea kupambana nje ya mahakama kwa kadri tunavyoweza ingawa tatizo litakuja iwapo Mahakama Kuu itaridhia kuisajili hukumu ya ICC na kuitaka TANESCO kulipa kwani hapo tozo hiyo itakuwa ikiongezeka kwa kiwango cha asilimia 7.5 kadri tutakavyokuwa tukichelewa kulipa,” alisema kiongozi huyo.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo ya ICC ambayo Tanzania Daima Jumatano imeipata nakala yake, kwenye ukurasa wa 89 majaji watatu waliotoa uamuzi huo, walitamka kuitambua Richmond Development Company LLC kuwa ni kampuni halali kwa mujibu wa sheria za Texas, Marekani.

Majaji hao, Gerald Aksen aliyekuwa Mwenyekiti wa Jopo anayetokea Marekani, Swithiri Munyantwali (Uganda) na Jonathan Parker (Uingereza) walitamka kwamba kuiita Richmond kuwa ni kampuni hewa ilikuwa ni kosa la kutafsiri isivyo sheria za Texas.

Katika kukazia hukumu hiyo ya ICC, majaji hao watatu walitumia hukumu mbalimbali za siku zilizopita zilizotumia kile walichokieleza kuwa ni ‘parol evidence’ katika kuhalalisha uwepo wa Richmond kisheria huko Texas.

Maamuzi hayo ya ICC kutamka katika hukumu yake kwamba Richmond ni kampuni halali na ilikuwa ni jina la kibiashara la kampuni ya RDEVCO, LLC yanapingana na yale yaliyotolewa na Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, katika kuichunguza kampuni hiyo.

Wakati ICC ikikubaliana kwamba Richmond Development Company, LLC ni jina la kibiashara la RDEVCO, LLC, Kamati Teule ya Bunge katika ripoti yake ilieleza bayana kwamba, uchunguzi wake walioufanya Texas kwa kushirikiana na taasisi za kisheria za huko ulithibitisha kwamba kampuni hiyo ilikuwa haina hadhi ya kuwa kampuni halali.

Katika eneo moja Kamati Teule ya Bunge ilieleza: “Kamati Teule imejiridhisha kuwa hakuna kampuni yenye jina la Richmond Development Company LLC iliyokuwa imesajiliwa Jimbo la Texas wakati wa kusaini mkataba huo au iliyosajiliwa baada ya mkataba huo hadi tunapowasilisha ripoti hii.

“Hitimisho tulilofikia linashabihiana kwa vigezo vyote na ushauri wa kitaalamu uliotolewa na kampuni mashuhuri ya mawakili ya Virginia, Marekani inayoitwa Hunton & Williams LLP kwa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO mwezi Oktoba 2006. Katika ripoti yake yenye jumla ya kurasa 19, kampuni hiyo ya mawakili imetamka bayana kuwa hakuna kampuni yenye jina la Richmond Development Company LLC kwenye masijala ya Katibu wa Jimbo la Texas ambaye moja ya majukumu yake ni sawa na ya Msajili wa Makampuni wa Tanzania.

“Nchini Marekani vilevile, huwezi ukakurupuka tu na kuanza kutumia jina mbadala la biashara bila kupitia usajili maalum ambao unawawezesha watu wengine kukagua jalada la majina hayo mbadala kwa lengo la kupata utambulisho kamili wa wanayoyatumia. Vilevile, sheria zinalazimu majina hayo kuchapishwa magazetini kwa lengo la kuutaarifu umma. Lengo, kama tulivyodokeza awali, ni kulinda raia wema dhidi ya vitendo vya udanganyifu.

“Katika Jimbo la Texas… ni kosa la jinai kutumia jina mbadala bila kulisajili. Usajili wa jina mbadala unadumu kwa miaka mitano ambapo mtumiaji lazima asajili jina hilo upya kati ya tarehe 1 Januari na 31 Disemba ya mwaka wa tano,” ilihitimisha Kamati Teule ya Bunge.

Tofauti ya maelezo na hitimisho kati ya Kamati Teule ya Bunge na ICC inaliweka sakata zima la Richmonda na mrithi wa mkataba wake Dowans katika hatua ambayo inaonyesha ukweli halisi wa jambo hili bado haujawekwa bayana.

Kwa maelezo mengine, tofauti hii inayafanya maneno aliyoyatoa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, wakati akihutubia wiki iliyopita eneo la Makuburi jijini Dar es Salaam kuwa na maana kubwa.

Dk. Slaa katika maelezo yake alitaka uchunguzi wa kina ufanywe kuhusu jambo hili na akafikia hatua ya kueleza kuwa, iwapo Kamati Teule ya Bunge ilisema uongo kuhusu uhalali wa Richmond basi hatua zinapaswa kuchukuliwa.

Mbali ya hiyo ICC katika ukurasa wa 41 wa hukumu yake hiyo inasema taratibu za kuhamishwa kwa mkataba kutoka Richmond kwenda Dowans zilizingatiwa kwani ziliridhiwa na TANESCO.

Katika ukurasa wa 44, ICC inaeleza kuwa Desemba 4, 2006 Dowans Holdings SA (Costa Rica) iliiandikia barua TANESCO ikieleza kwamba ilikuwa inakusudia kuanzisha na kusajili kampuni nchini itakayoendesha na kusimamia utekelezaji wa majukumu ya RDEVCO.

Hukumu hiyo katika ukurasa wa 54 inaonyesha kwamba, Desemba 21, 2006, TANESCO waliridhia uhamishwaji wa mkataba wa Richmond kwenda Dowans hali ambayo iliiwezesha kampuni hiyo ya Costa Rica kuanza kuzalisha umeme wa awali wa megawati 20 kuanzia Januari 26, 2007.

Hata hivyo kabla ya TANESCO kuridhia, ICC inakiri kwamba moja ya benki nchini Canada ya Citibank ilipata kukanusha kuwa na mahusiano yoyote na Dowans.

ICC katika hukumu kwenye ukurasa wa 120 ilifikia hatua ya kupingana na maelezo ya awali yaliyokuwa yakiiondolea uhalali Dowans kutokana na mkataba wake kusainiwa kinyume cha matakwa ya Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPA).

Majaji hao watatu wa ICC mbali ya kupinga hoja za TANESCO kwamba mkataba ulioingiwa kinyume na PPA ulikuwa ni batili, walikwenda mbele zaidi na kueleza kuwa tafsiri ya namna hiyo ya sheria inaweza ikawa na madhara makubwa kwa jamii na wananchi wasio na hatia wanaohitaji huduma ya umeme.

Kitendo cha ICC kupingana na hoja za ukiukwaji wa PPA kinakwenda kinyume cha msingi wa ushauri ambao TANESCO ilipewa na kampuni ya Rex Attorneys walioshauri kuvunjwa kwa mkataba wa Dowans.

Tafsiri hii ya ICC inaibua hoja nyingine ya Dk. Slaa ambaye katika kauli yake hivi karibuni ametaka ufanyike uchunguzi wa kina juu ya Rex Attorneys ambao ndio walioishauri TANESCO kuvunja mkataba huo na wao wenyewe wakashindwa kwa hoja katika kulitetea shirika hilo katika mahakama hiyo ya kimataifa.

Chanzo cha habari: Tanzania Daima 2 Februari 2011

Advertisements

Written by simbadeo

February 2, 2011 at 10:30 am

Posted in Siasa na jamii

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: