simbadeo2000

WAZA MPAKA BASI (THINK TO NO END).com weblog NOTE: Views or opinions expressed in this blog do NOT in any way represent those of any organisation, community, association, company, circle of friends, religious or ethnic group to which I am associated with.

Idd Simba: Amani inatoweka …

with one comment

Mchoro na: Cloudy Chatanda

Idd Simba: Nchi ipo hatarini

na Salehe Mohamed

MSHAURI wa jopo la masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Iddi Simba, amesema nchi ipo hatarini kwa sababu amani na utulivu wa Tanzania vimeanza kutoweka.

Simba aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara katika Serikali ya Awamu ya Tatu, aliyejiuzulu kutokana na kashfa ya utoaji wa vibali vya sukari, alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati jopo hilo likizungumza na waandishi wa habari kuhusu mustakabali wa taifa.

Alisema kuwa ni vema amani na utulivu uliopo vikaenziwa badala ya watu kutoa kauli za kuchochea vurugu za kisiasa na kidini.

“Kila neno linalotolewa na wanasiasa au viongozi wa dini lina uzito wake, tunaonya amani na utulivu vimeanza kutuponyoka ni vema tukawa makini,” alisema.

Alibainisha kuwa jopo hilo si kundi la wababishaji au lenye kutafuta madaraka katika jamii bali ni la watu makini wasiopenda kubezana, kukejeliana na vitendo vingine vyenye lengo la kuigawa jamii.

Awali kabla ya Simba kutoa kauli hiyo, mratibu wa jopo hilo, Sheikh Mohamed Idd Mohamed, alitoa tamko la kuwataka viongozi wa vyama vya siasa kutomkebehi na kumkejeli Rais Jakaya Kikwete.

Sheikh Mohamed alisema kejeli na kebehi hizo hazisaidii kuimarisha amani na demokrasia bali zinavunja.

Alisema wananchi hawana budi kuzingatia utawala wa sheria na kutii amri za mamlaka zilizoundwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.

“Jopo la masheikh linawaasa Watanzania kuzingatia utawala wa sheria na kutii amri za mamlaka zilizoundwa kwa mujibu wa sheria za nchi na linatabanaisha kuwa kupinga amri za mamlaka za kisheria ni kupinga amri za Mwenyezi Mungu aliyeziweka,” alisema.

Sheikh huyo aliongeza kwamba ni kosa kutoitii mamlaka hiyo, ni kusababisha uvunjifu wa amani na kupoteza roho na mali kama ilivyotokea Arusha hivi karibuni.

Katika maelezo yake, alisema wamesikitishwa na kauli ya maaskofu zilizoonyesha kuunga mkono matakwa ya chama cha siasa na kufikia kutomtambua kiongozi wa kisiasa kwa misingi ya kisiasa.

Alisema viongozi hao wanasahau wao ni viongozi wa dini yao na wala si viongozi au wasemaji wa vyama vya siasa.

Jopo hilo limewataka maaskofu kuacha mara moja mwenendo huo mbaya unaoweza kuwagawa viongozi wa vyama vya siasa, wanasiasa na watendaji wa serikali kwa misingi ya dini na kuisambaratisha nchi.

Aliwataka maaskofu kuacha mara moja mwenendo huo mbaya unaoweza kuwagawa viongozi wa kisiasa na watendaji wa serikali kwa misingi ya kidini, na kusambaratisha nchi vipande vipande.

Aidha, kwa upande mwingine linampongeza Rais Kikwete kwa kuona umuhimu wa kuunda Tume ya Katiba.

Sheikh Mohamed, alisema jopo hilo linampongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuona umuhimu wa kuunda Tume ya Katiba ambayo wanaamini itafanya kazi itakayokidhi matarajio ya Watanzania.

Chanzo: Tanzania Daima, 20 Januari 2011.

TAFAKARI BINAFSI

Hivi kwa nini hivi sasa tunazungumza sana habari za udini? Hivi ni lazima sana kuzungumzia udini? Hatuwezi tu kuamua kuendelea na shughuli zetu bila kujizungumzisha na mambo ya udini? Hivi muda huu wa kulumbana kuhusu ‘udini’ wetu tunaupata wapi sisi badala ya kujenga uchumi wa nchi na kuwaandalia vizazi vya sasa na vijavyo nchi madhubuti?

Hebu tufikirie, ni mangapi ya ‘maana’ yanatusubiri? Tujenge nchi jamani. Haya ya ‘udini’ tutakutana nayo ahera … hapa tunatakiwa kuchapa kazi … ni kazi tu kwa kwenda mbele! Maana mambo ukiyazungumza saaaaana, ukiyaandika saaaana, ukiyatangaza saaaana … basi ujue ndiyo unafanya kazi ya kupandikiza chuki za kidini … Maana watoto si wanasikia, vijana si wanaona? Yanawaingia akilini. Jambo likimwingia binadamu akilini tangu umri mdogo … hakuna wa kulibandua … hata ulete grader au kifaru … haling’oki ng’o! Tunawalisha nini watoto na vijana wetu?

Naudhika sana kila mara nikisoma au kusikia habari za ‘fulani analeta udini, fulani anatumia dini’. Hebu tuchape kazi. Dini hukohuko makanisani, misikitini, masinagogini, chini ya miti mikubwa, kwenye vijumba vya kinyamkera, kwenye mapango … hukohuko … siyo hapa kwenye jamii. Nani anataka Frantz Fanon aamke huko aliko na kuja kutucheka … maana yote haya aliyatabiri katika The Wretched of the Earth. Hizi dini za ‘kupokea’ ambazo Afrika imezidaka kutoka wa wakoloni/wakamata watumwa … zitakuja kuligawa bara, zitakuja kuleta vita na mapigano makubwa ya wenyewe kwa wenyewe … yameshatimia kule Nigeria, yametokea kule Uganda, yametokea na yanaendelea kutokea kula Sudan/Darfur … na kwingineko unakoweza kufikiria.

Advertisements

Written by simbadeo

January 20, 2011 at 2:24 pm

Posted in Siasa na jamii

One Response

Subscribe to comments with RSS.

  1. Ni kweli kabisa kaka simba kama ulivyosema watu tuchape kazi kwa bidii, na sikukaa na kujadili mambo ya udini kila kukicha, hebu tukae kimya tuone kama hivyo vita vya udini vitatokea!! Lakini tukiendekeza maneno yasiokuwa na maana vinywani mwetu ni kweli kabisa vitatokea.

    Like

    dorine

    January 20, 2011 at 2:47 pm


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: