simbadeo2000

WAZA MPAKA BASI (THINK TO NO END).com weblog NOTE: Views or opinions expressed in this blog do NOT in any way represent those of any organisation, community, association, company, circle of friends, religious or ethnic group to which I am associated with.

Kutoka Tanzania Daima Jumapili …

with one comment

Tafakari … Tanzania na safari yake ya kukua kama nchi ya kidemokrasi … uwazi … ukweli … uthubutu … na nia za kweli za kusaidia Taifa dhidi ya zile za kukidhi kiu binafsi …


Sitta, Lowassa waitesa CCM

• Vita vya urais, makundi yashamiri

na Bakari Kimwanga

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kiko katika wakati mgumu wa kudhibiti makundi ya makada wake ambao wameanza vita vya kuwania madaraka na malumbano yanayotafsiriwa kukiweka njia panda chama hicho kikongwe, Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa.

Miongoni mwa makada wanaonekana kukipa wakati mgumu chama hicho ni aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ambaye wiki hii aliibuka na kauli nzito iliyopingwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusufu Makamba.

Mwanasiasa mwingine anayeonekana kukiumiza kichwa chama hicho ni spika wa zamani wa Bunge na Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ambaye kauli zake za siku za hivi karibuni zimeibua maneno mengi ya chini chini na ya wazi.

Wakati Lowassa ameingia katika mzozo na Makamba kutokana na kauli yake ya kuvitaka vyama vya CCM na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukaa pamoja na kumaliza tofauti zao zilizosababishwa na mzozo wa umeya katika mji wa Arusha, Sitta ameibua mjadala baada ya kudai kwamba alienguliwa katika mchuano wa uspika kutokana na hofu ya viongozi wa juu wa CCM walioshindwa kwenda sambamba na kasi na viwango vyake.

Makamba katika matamshi yake dhidi ya Lowassa, alipinga wazo la kukutana na CHADEMA kujadili mzozo huo akisema chama chake kilikuwa hakina sababu ya kufanya hivyo kutokana na ukweli kwamba kilikuwa kimeshinda kihalali kinyang’anyiro cha umeya wa Arusha.

Kama hiyo haitoshi, Makamba alieleza kushangazwa na kitendo cha Lowassa kutoa matamshi hayo hadharani wakati akiwa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ambako ndiko alikokuwa akipaswa kuwasilisha hoja yake hiyo.

Lowassa kwa upande wake aliieleza Tanzania Daima kwa simu juzi kushangazwa kwake na matamshi ya Makamba dhidi yake akisema lilikuwa ni jambo lisiloingia akilini kwa kiongozi wa juu wa CCM kukataa kukaa meza moja na CHADEMA wakati akijua kwamba chama hicho kimekaa katika meza ya mazungumzo na Chama cha Wananchi (CUF) katika mzozo wa Zanzibar.

“Nimeshangazwa na Makamba kwa sababu anaona hakuna sababu ya kuzungumza na CHADEMA kuhusu mzozo wa umeya Arusha ambao katika kauli yangu niliwaonya wanasiasa kutojaribu kuugeuza mji huo kuwa Ivory Coast nyingine. Mbona katika mzozo wa Zanzibar tumekaa na CUF kwa nini iwe vigumu kuzungumza na CHADEMA?” alihoji Lowassa.

Kwa upande wake, Sitta anaingia katika mzozo na makada wenzake ndani ya CCM kutokana na kile ambacho baadhi yao wanakiona kuwa ni kinyongo dhidi ya wanachama wenzake ambao anaamini ndiyo waliokuwa na mkono katika kuenguliwa kwake katika nafasi ya uspika aliyoishikilia kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Inadaiwa kuwa kutokana na kinyongo hicho Sitta, anawatuhumu makada hao kuhusika na kashfa mbalimbali za ufisadi ikiwemo ile ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond ambayo mkataba wake wa kulipwa kiasi cha sh milioni 152 kwa siku ulirithiwa na Dowans Tanzania Ltd.

Sitta, hivi karibuni, aliitaka serikali isilipe kiasi cha sh bilini 185, ilizoamuliwa iilipe kampuni ya Dowans baada ya kuvunja mkataba wa kununua umeme na kampuni hiyo.

Kutokana na hatua ya Sitta, kutoa kauli za utata, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Hamis Mgeja, ameweka wazi nia yake ya kupeleka hoja za kumshitaki kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC).

Mgeja anamtuhumu Sitta, kwa kuendeleza mgawanyiko ndani ya CCM huku akimtaka kufuta kauli yake kuwa aliondolewa kugombea uspika kwa mizengwe na Kamati Kuu ya chama hicho tawala.

Mapema wiki hii, Mgeja, alimjia juu Sitta, akimtuhumu kwa kuendeleza mgawanyiko ndani ya CCM huku akimtaka kufuta kauli yake kuwa kuondolewa kugombea uspika aliondolewa kwa mizengwe na Kamati Kuu ya chama hicho tawala.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili kwa njia ya simu Khamis Mgeja, alisema kuwa yeye kama kada mwaminifu wa CCM, anajua nachokifanya Sitta, kwani hivi sasa ameanza mipango yake ya urais kupitia Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM).

Akizungumzia kwa undani mipango hiyo ya Sitta, na kundi lake alisema hivi sasa wameamua kuanza maandalizi hasa kwa kumuandaa mmoja wa vigogo katika serikali ili agombe urais Mwaka 2015, kwa kupitia nguvu ya vijana.

“Mimi ni kada mwaminifu kwa chama changu na msimamo wangu wa kuwasilisha hoja utabaki palepale ni lazimka Sitta, aeleze ukweli ndani ya vikao, na ninajua hivi sasa yeye na kundi lake wameanza maandalizi ya kumuandaa mmoja kati ya kigogo ili awanie nafasi ya urais mwaka 2015,” alisema Mgeja.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili jana, Sitta, alisema alikuwa akimtakia baraka Mgeja katika hoja yake hiyo ambayo amesema ina mikono ya watu wengine nyuma yake.

“Sina cha kusema katika hilo, ila namshangaa Mgeja acha aendelee na mipango yake ambayo ninajua nyuma yake kuna kina nani, ila ipo siku nitasema kama anahitaji niseme,” alisema Sitta.

Ukiacha kauli hiyo ya Sitta, nyingine ambayo imeibua mjadala ni ile inayohusu Dowans ambayo aliitoa siku chache baada ya kutolewa kwa hukumu na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kimataifa (ICC) ambayo iliipa ushindi kampuni hiyo dhidi ya TANESCO iliyotakiwa kuilipa faini ya shilingi bilioni 185.

Katika hilo Sitta, alisema hukumu ya Dowans dhidi ya TANESCO ni mbinu zagenge la mafisadi watatu (ambao hakuwataja kwa majina) wanaohujumu nchi kuandaa mpango wa kutafuta fedha kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Waziri Sitta, alisema ataendelea kupambana na ufisadi hata kama kuna mbinu chafu zinafanywa dhidi yake na mafisadi ambao anaamini hawatafanikiwa kwa sababu hawaungwi mkono na watu wengi.

Alisema genge hilo ambalo halina huruma na nchi na umaskini wa Watanzania na kama likiachwa lijiimarishe, Watanzania wasubiri matatizo makubwa zaidi huko mbele.

Sitta ambaye katika bunge la tisa alikuwa Spika aliyeruhusu mjadala mkali kuhusu kampuni ya kufua umeme ya Richmond iliyosababisha Lowassa, kulazimika kujiuzulu uwaziri mkuu na kisha akafuatiwa na mawaziri wengine wawili, alisema kinachofanyika sasa ni genge hilo kujiandalia mazingira ya kujikusanyia mabilioni ya fedha chafu za uchaguzi wa 2015.

Sitta alionya na kuwataka Watanzania kutofanya mchezo kwa kuwa macho na genge hilo ambalo alisema limekuwa na mazoea mabaya hali iliyopelekea taifa kuwa katika wakati mgumu hasa katika ulipaji wa fidia wa Dowans.

Alisema kwa kutumia nafasi yake kama waziri atajitahidi hasa kwa kushauriana na mamlaka za serikali ili kuzua hali hiyo yoyote yenye dalili ovu kwa taifa.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Sitta ilipingwa kwa nyakati tofauti na Mwanasheria Mkuu wa kwanza, Jaji Mark Bomani na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambao walisema itakuwa ni jambo gumu kutoilipa Dowans hasa iwapo hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji itasajiliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

Wachambuzi wa mambo ndani na nje ya CCM wanaielezea mizozo hiyo inayowahusisha Lowassa na Sitta katika maeneo tofauti ikiwa ni pamoja na mtikisiko unaoukumba Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), kuwa ni dalili za mwanzo za vita ya urais wa mwaka 2015.

Baadhi ya makada waliopo ndani ya chama hicho, wamelidokeza Tanzania Daima Jumapili, kuwa hivi sasa kuna vita kubwa ya uongozi ndani ya CCM, ambapo vigogo wa chama hicho wamekuwa wakihaha kuunda mitandao itakayowasaidia kutimiza malengo yao Walidokeza kuwa hata UVCCM kuna hali tete licha ya Katibu Mkuu wake Martin Shigela kupinga jambo hilo kwa madai kuwa linachochewa na watu fulani kwa malengo binafsi Chanzo hicho kilidokeza kuwa UVCCM, hivi sasa kimemeguka ambapo yapo makundi yanayolenga kuwaandalia mazingira mazuri baadhi ya makada ili wawanie rais mwaka 2015 au ujumbe wa vikao vya juu vya chama utakaofanyika mwaka 2012.

Source: Tanzania Daima Jumapili, 26 Desemba 2010

Advertisements

Written by simbadeo

December 26, 2010 at 11:25 am

Posted in Siasa na jamii

One Response

Subscribe to comments with RSS.

  1. Hiii ni kawaida CCM kulumbani mwisho wa siku hakuna la maana kitakalo tokea

    Like

    Jumanne Nyakirang'ani

    June 8, 2014 at 8:48 am


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: