simbadeo2000

WAZA MPAKA BASI (THINK TO NO END).com weblog NOTE: Views or opinions expressed in this blog do NOT in any way represent those of any organisation, community, association, company, circle of friends, religious or ethnic group to which I am associated with.

Kikwete … ukimya wa vyombo vya habari

leave a comment »

Hapa chini nawaletea habari kutoka Tanzania Daima lilivyoripoti juu ya kuanguka kwa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Mh. Dkt. J. M. Kikwete. Kwa kuwa vyombo vingi vya habari vilikuwa kimya kuhusu tukio hili, si vibaya Watanzania wakapata fursa ya kusoma na walau kufahamu nini hasa kilitokea. Si vema kuruhusu minong’ono. Ni afadhali kuripoti kama hali ilivyokuwa kuliko kuinyamazia. Ndiyo hekima inavyoelekeza.

Kikwete aanguka tena
• CCM yasema ni kutokana na sukari kushuka
na Waandishi wetu

SHEREHE za uzinduzi wa kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilizoanza jana katika viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam ziliingia dosari baada ya mgombea wa urais wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, kuishiwa nguvu na kuanguka jukwaani wakati akihutubia.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa 10:20 jioni, ikiwa ni muda usiozidi dakika 15 tangu alipopanda jukwaani na kuanza kuhutubia umati mkubwa wa wakazi wa Dar es Salaam waliofika katika sherehe hizo.

Dalili za Kikwete kuishiwa nguvu na kuyumba zilisababisha wasaidizi wake wawili waliokuwa nyuma yake kumdaka na kumnusuru kufika sakafuni kabla ya kundi la maofisa wa usalama kumzingira, kumbeba na kumpeleka nyuma ya jukwaa alikopatiwa huduma ya kwanza.

Wakati akifikwa na masaibu hayo, Kikwete alisikika akitamka neno moja tu la mwisho ‘aise’ na sekunde chache baadaye hali ikawa ya ukimya katika viwanja hivyo, tukio lililofuatiwa na hatua ya Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, kuwataka wananchi watulie huku akimalizia maneno yake kwa kusema ‘Mungu yupo.’

Ilichukua muda wa dakika 20 kwa Kikwete kupatiwa matibabu kabla ya kurejea uwanjani kuendelea na hotuba yake kwa muda wa dakika zipatazo tatu na kisha akatangaza kuzinduliwa kwa kampeni na akaenda kukaa katika kiti chake.

Alipopanda jukwaani na kuanza kuhutubia tena, Kikwete alianza kwa kusema: “Nimefungulia jamani…niliishia hapa kwenye…naona wamevuruga hotuba yangu” na akaendelea kueleza kuhusu mafanikio ambayo serikali yake imepata, huku akinywa maji kwa zaidi ya mara moja.

Wakati wote Kikwete alipokuwa akipatiwa huduma ya kwanza, hali katika jukwaa kuu ambako walikaa viongozi wakuu na wastaafu ilikuwa ni ya ukimya mkubwa na kwa kipindi kirefu, Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, alionekana akiwa ameshika tama kwa mkono wake wa kushoto.

Wengine walioonekana wakiwa katika hali ya simanzi walikuwa ni, Makamu wa Rais, Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, Rais mstaafu, Benjamin Mkapa na waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa.

Maelfu ya wananchi waliojitokeza katika viwanja hivyo kufuatilia kampeni hizo za CCM walikuwa katika hali ya ukimya na kusubiri kusikia hatima ya hali ya afya ya kiongozi mkuu wa taifa, huku baadhi yao wakiangua vilio vya kwikwi.

Hali katika viwanja hivyo ilikuwa ni ya mashaka makubwa, kwani muda mfupi baada ya Kikwete kuondoka uwanjani hapo majira ya saa 10:50 jioni, maofisa usalama waliwatia nguvu baadhi ya watu akiwamo mwandishi wa habari wa kujitegemea wa gazeti hili, Bakari Kimwanga, kabla ya kumuingiza katika gari aina ya Land Rover lenye namba za usajili STJ 6157.

Tukio la jana lilikuwa ni la tatu kwa Kikwete kuishiwa nguvu na kuanguka jukwaani katika kipindi cha miaka mitano baada ya kufikwa na hali hiyo kwa mara ya kwanza katika viwanja hivyo hivyo vya Jangwani mwaka 2005.

Kikwete alifikwa na tukio la aina hiyo pia, Oktoba mwaka jana jijini Mwanza wakati akihutubia katika Uwanja wa CCM Kirumba, wakati akihutubia mamia ya wananchi waliokusanyika kusherehekea miaka 100 ya kuanza kwa Kanisa la African Inland (AIC).

Akizungumza na wana habari katika ofisi ndogo za Makao Makuu ya CCM jijini Dar es Salaam jana jioni kuelezea kuhusu tukio hilo la Kikwete kuanguka, mkuu wa kitengo cha habari cha kampeni za CCM, Kanali mstaafu, Abdulrahman Kinana, alisema kilichosababisha hali hiyo ni upungufu wa sukari, kulikosababisha kushuka kwa shinikizo la damu.

“Kwa mujibu wa madaktari wake, sababu kubwa iliyosababisha tukio la leo ni upungufu wa sukari mwilini na kushuka kwa pressure, kwa sababu alikuwa amefunga,” alisema Kinana wakati akitoa maelezo yanayoshabihiana na yale ya mwaka 2005, ambayo pia yalihusisha tukio la Kikwete kuanguka kwa sababu ya mfungo.

Kinana alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wanachama, wapenzi na mashabiki wa CCM kwamba hali ya afya ya Kikwete ilikuwa njema na ataendelea na ziara yake ya kampeni leo hii mkoani Mwanza na kwingineko nchini.

Mbali ya hilo, Kinana alisema uamuzi wa Kikwete kufunga ulikuwa ni kinyume cha ushauri aliopewa na madaktari wake ambao walishauri asifunge.

Alisema tayari chama hicho na madaktari wake wameshachukua hatua zote za tahadhari ili kuhakikisha kuwa mgombea huyo wa urais anaendelea na kampeni zake za urais pasipo kukwama.

Katika hatua nyingine, mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, jana alimtumia Rais Kikwete salamu za pole kutokana na tukio la kuanguka kwake.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Dk. Slaa, alisema aliamua kumtumia salamu za pole Rais Kikwete kwa kuwa Watanzania wote ni ndugu na siasa si uadui.

Alisema kuwa anakumbuka kuwa Rais Kikwete alimtumia yeye (Slaa) salamu za pole aliposikia kuwa amevunjika mkono baada ya kuanguka bafuni mkoani Mwanza.

“Mheshimiwa Rais nimepokea kwa masikitiko taarifa ya hali ya afya iliyokupata Jangwani leo, nakuombea sana upate nguvu haraka hasa katika kipindi hiki kigumu, nakupa pole sana sana.” Alisema Dk. Slaa katika ujumbe mfupi aliomtumia Kikwete.

Chanzo: Tanzania Daima 22.08.2010

Advertisements

Written by simbadeo

August 22, 2010 at 12:40 pm

Posted in Siasa na jamii

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: