simbadeo2000

WAZA MPAKA BASI (THINK TO NO END).com weblog NOTE: Views or opinions expressed in this blog do NOT in any way represent those of any organisation, community, association, company, circle of friends, religious or ethnic group to which I am associated with.

SUMATRA … kazeni buti …

leave a comment »

Matukio ya ajali nchini Tanzania yanazidi kuongezeka. Kuna ripoti ya ajali iliyotokea Nzega jana na kuua watu wapatao 24 na kujeruhi wengine wengi. Tukio hili na mengine ya aina hiyo yanatia si tu simanzi na huzuni peke yake bali yanalisababishia Taifa letu hasara kubwa ya maisha ya watu pamoja na uharibifu wa mali zao.

Mnamo tarehe 24 hadi 25 Februari mwaka huu nilisafiri kwa basi linalokwenda kwa jina la Mabrouck kutoka Tabora kuja jijini Dar es Salaam. Tuliyoyaona na kuyapitia abiria si mageni kwa wasafiri wa barabara hapa nchini. Huduma za mabasi yaliyo mengi bado ni duni sana. Biashara inaendeshwa kiholela mno. Hakuna ratiba rasmi wala mtu unayeweza kuwasiliana naye akakupa utaratibu maalumu ulivyo na pale kunapotokea namba ya siti kugongana au basi kutoondoka katika muda ulioandikwa kwenye tiketi, hupati hata mtu mmoja anayehusika wa kutoa suluhu au kutolea jambo hilo maelezo.

Linapokuja suala la mwendo kasi – abiria mkipiga kelele mwendo upunguzwe – kweli unapunguzwa – lakini ni kwa muda tu – baada ya hapo mwendo mdundo kama kawa – si kwenye mashimo ya barabara za vumbi, kwenye barabara zinazopita vijijini na miji midogomidogo wala matuta kwenye barabara za lami.

Basi tulilosafiria lilipaswa kuondoka saa 1 asubuhi siku ya Jumatano, lakini kwa sababu ambazo mmiliki na wafanyakazi wake wanazielewa wao basi liliondoka saa 7.30 mchana. Jambo hili lilizua mzozo mkubwa kati ya abiria na baadhi ya wafanyakazi waliokuwepo kwenye ofisi za basi hilo la Mabrouk – baadhi ya wafanyakazi hao walitambuliwa kwa majina ya Suzy, Hamis na Jumanne. Baadaye nao waliyeyuka kiaina na kuiacha ofisi bila mhudumu yeyote.

Basi hilo lilipofika Singida mjini liligonga kizuizi cha barabarani cha polisi – ilikuwa yapata saa 1 usiku – hivyo kusababisha basi kukamatwa na kushikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Singida. Jinsi wafanyakazi wa basi hilo walivyolimaliza tatizo hilo pale polisi wanajua wao na maafisa wa polisi – lakini tuliruhusiwa kuondoka pale majira ya saa 2.30 usiku. Tuliingia Dodoma mjini saa 7 usiku. Tulilala (kesha) pale Dodoma na kuanza tena safari majira ya saa 11 alfajiri.

Basi lilifika Morogoro – eneo la Msamvu – majira ya saa 2.15 asubuhi. Hapa tena dereva wa basi letu alifanya kituko – alikwenda kupaki nje ya Kituo cha Mabasi cha Msamvu – hivyo kufanya ‘wrong parking’ – matokeo yake tena wakapata mzozo wa kutozwa faini na maafisa wanaohusika na usimamizi wa Kituo hicho cha mabasi.

Dar es Salaam tuliingia saa 6 mchana – tukiwa hoi bin taabani – kwa kurushwarushwa na basi, kwa barabara mbovu, kwa uchakavu wa ndani ya basi na kwa kughasiwa kiakili na huduma mbovu ya kampuni inayomiliki mabasi ya Mabrouk.

Ndiyo sababu ninasema – ipo haja kubwa sana kwa SUMATRA na maajenti wao wakishirikiana na Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani kuwa ‘serious’ zaidi na kazi yao, wakaze buti. Kampuni kama hiyo inayomiliki mabasi ya Mabrouck ichunguzwe na ikiwezekana inyang’anywe leseni ya biashara maana sidhani kama inakidhi masharti ya leseni ya biashara hiyo.

Kero nyingine niliyoshuhudia ni ugonganishaji wa namba za siti – siti moja inakuwa imepangiwa abiria wawili mpaka watatu. Utaratibu mbovu wa uuzaji wa tikiti. Matokeo yake baadhi ya abiria walilazimika kusafiri huku wamesimama – fikiria kusimama kutoka Tabora hadi Dar es Salaam. Ni adha na mateso makubwa.

Pia ile kupoteza muda wa kuanza safari – peke yake ni tatizo – maana kama tungeondoka katika muda uliopangwa, si ajabu kwamba tungefika Dar siku hiyohiyo usiku. Kesho yake watu wangeingia kwenye shughuli zao za kila siku. Lakini ucheleweshaji ule tayari uliongeza gharama kwa wasafiri, uliowapotezea muda ambao ungetumika kwa uzalishaji n.k. Kwa hiyo, Taifa linaingia hasara kubwa. Fikiria kama abiria 50 wameharibiwa muda wao je hiyo ni hasara kubwa kiasi gani kwa Taifa. Hilo ni basi moja. Je, kwa nchi nzima yanasafiri mabasi mangapi? Hasara ni kubwa.

Nawasilisha.

Ofisi ya mabasi ya Mabrouck ya mjini Tabora

Basi la Mabrouck likiwa limejaza abiria kupita kiasi … tamaa … uendeshaji biashara kiholela…

Uchakavu ndani ya basi … hata kama tunaishi ulimwengu wa tatu bado tunastahili kusafiri kwenye vyombo vilivyo na viwango bora zaidi kuliko hivi.

Basi la Mabrouck lilipofanya ‘wrong parking’ pale Msamvu, Morogoro

Baadhi ya wanaohusika na mabasi ya Mabrouck, wa kwanza kushoto alitambulika kwa jina moja la Suzy, wakati huyo wa mkono wa kulia jina lake halikufahamika mara moja ila alikuwa miongoni mwa watoa maelezo kuhusiana na kuchelewa kuondoka kwa basi.

Advertisements

Written by simbadeo

March 2, 2010 at 4:19 pm

Posted in Siasa na jamii

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: