simbadeo2000

Dhahabu safi …

Mar 27
1 Comment

barabaramtoni.jpg

Mafundi wakiwa bize kujaribu kuzuia mmomonyoko zaidi katika barabara iendayo Mbagala, eneo la Mtoni. Barabara ilimegwa na maji ya mvua zilizonyesha siku ya Jumatano na Alhamisi wiki hii. Tatizo hilo lilisababisha ugumu usiosemekana wa usafiri, kwani magari hapo yalitumia hadi saa 2 kupita eneo hilo kabla ya kukumbana na tatizo la foleni kwenye barabara hiyo.

barabaramtoni3.jpg

Sehemu ya barabara ya Kichangani inayoungana na ile ya Mbagala pale mtoni ikiwa imekatika kipande kikubwa kiasi cha kufanya magari yashindwe kupita.

barabaramtoni2.jpg

Upande wa pili wa barabara hiyo ya kichangani pale Mtoni.

Inasemekana kwamba dhahabu safi ni ile inayojaribiwa kwa kupitishwa katika tanuru la moto. Ikiwa kipande cha dhahabu kitapita salama katika tanuru hiyo, basi hiyo huwa ni dhahabu safi. La kikiungua na kubaki majivu, basi haikuwa dhahabu.

Barabara hii haina miaka miwili tangu ijengwe. Mvua ya siku mbili imeikatilia mbali na kusababisha matatizo makubwa likiwemo lile la shida ya usafiri kwa watu wengi.

Ipo haja ya kukagua ipasavyo ubora wa barabara zinazojengwa sehemu mbalimbali za Dar es Salaam hivi sasa. Ulipuaji wa kazi ni wa kiwango cha juu. Tunaweza kusema kuwa huu ni ufisadi wa aina yake. Hii si haki. Barabara haina miaka miwili na tayari imekatika. Si haki kwa Watanzania wenye matumani ya Maisha Bora kwa kila mmoja wao.


Posted in Siasa na jamii

Kizaazaa cha mvua Bongo …

mvuadar2.jpg

Lilipotokea basi la abiria, wapo waliotamani hata kupanda juu ya keria. Hapa konda angetangaza nauli buku (1000/=) bado angejaza basi.

mvuadar3.jpg

Pale Mtava ilikuwa ni kizungumkuti. Barabara iligeuka bahari. Wenye magari mkweche yaliwazimikia pale. Si njia ya waenda kwa miguu wala ya wapanda baiskeli iliyopona. Ama kwa hakika, ipo kazi kubwa sana kwenye ulimwengu wa miundombinu na majengo tunayojenga karibu na barabara.

mvuadar27machi.jpg

Raia wengine wa Tanzania waliamu kukanyaga kwa mguu. Mvua ikiendelea kuwachapa bila huruma. Lo, mpaka lini?

mvuadar4.jpg

Abiria wakisota kituoni. 27 Machi 2008. Banda la Ngozi. Dar es Salaam. Tanzania.


Posted in Siasa na jamii

Kazi ya sanaa…

mrisho.jpg

Kazi ya sanaa ya Mrisho.  Ni moja ya kazi maridadi sana. Vipaji vipo Bongo. Tunachopaswa kufanya ni kufungua macho yetu na tutaona vipaji. Tuvienzi. Tuvidumishe. Tuviunge mkono.


Posted in Siasa na jamii

Pasaka Njema …

dscf0031air2.jpg

Ni saa moja usiku, Dar es Salaam, 21 Machi 2008.

Natumia fursa hii kuwatakia wadau wa blogu hii heri tele za sikukuu ya Pasaka. Taa hizo ziwe ishara ya mwanga unaotokana na Pasaka ili kuwaangazia njia hasa katika vipindi vigumu katika maisha.

Ujumbe wa Pasaka kutoka blogu hii: UKWELI UTAKUWEKA HURU.


Posted in Siasa na jamii

Sura ya Dar kutokea baharini …

Mar 09
1 Comment

darshiptower.jpg

utumishihouse.jpg

Inazidi kupendeza. Labda tatizo pekee ni harufu ya ufisadi. Naamini yangependeza hata zaidi kama kusingalikuwa na harufu hiyo ya ufisadi. Aah, ufisadi, kwa nini unanenepesha wachache na kuwakondesha mamilioni wengine? Mpaka lini utaendelea hivyo? Mpaka lini tuendelee kupaka chokaa na rangi makaburi ambayo ndani yake yamejaa uoza na mifupa?

Ufisadi, tokomea, tokomeaaaa!

Ondoka, unatutesa, unatunyanyasa katika nchi ya mababu na mabibi zetu wenyewe, ondoka, angamia.


Posted in Siasa na jamii

Kumbe ni ubunifu …

Mar 09
1 Comment

shaibu-issa.jpg

Anaitwa Shaibu Issa. Ni fundi wa kutengeneza ‘antena’ za TV kwa kutumia tube lights zilizoisha muda wake. Hutengeneza wastani wa ‘antena’ 10 kwa siku. Huuza wastani wa sita (6) kwa siku. Antena moja huiuza kati ya Tsh. 4,000 na 6,500.

Maoni yake ya jumla, watu wanazidi kuzikubali ‘antena’ za aina hii. Hii inadhihirishwa na idadi ya antena anazouza. Idadi inakwenda juu. Anatuhimiza Watanzania tutumie vile tunavyozalisha wenyewe hapa nchini. Tutoe kipaumbele kwa vitu hivyo kabla ya kufikiria kununua vya nje.

Kutokana na ubunifu huu, Issa anajitengenezea kipato ambacho anakitumia kwa kuendesha maisha yake na ya familia yake. Analipa kodi mbalimbali serikalini, kwa njia mbalimbali. Anasaida ‘kurecycle’ chupa hizo kwa njia yake.

Issa ni mjasiriamali. Vijana wengi wakileta ubunifu mbalimbali hatutakuwa na tatizo kubwa la ajira kama lilivyo hivi sasa. Tuendeleze ubunifu wa aina mbalimbali kwa kusupport Watanzania wenzetu wanaoleta ubunifu hizo.


Posted in Siasa na jamii

Akili ni nywele …

vingunguti1.jpg

vingunguti2.jpg

vingunguti3.jpg

vingunguti4.jpg

Ilikuwa ni fujo tupu pale eneo la Vingunguti jioni ya tarehe 6 Machi 2008. Picha ya kwanza juu inaonyesha chanzo cha vurugu hizo za magari. Daraja hilo kwa ajili ya matangazo mbalimbali lilikuwa likifungwa/likijengwa.

Matokeo ya kazi hiyo, kama ilivyokutwa mnamo saa 11.40 jioni ni pamoja na msongamano mkubwa wa vyombo vya moto na hata matatizo kwa waendao kwa miguu kupitia Barabara ya Nyerere katika eneo hili la Vingunguti.

Ilikuwa adha kubwa. Hata matrafiki waliojaribu kuweka mambo sawa hawakumudu. Ilikuwa kana kwamba hawapo. Madereva walijichukulia uamuzi wa kupita popote. Wapo waliopita katika lane zisizo zao, mithiri ya Bush na msafara wake, kama unavyoona katika baadhi ya picha hapo juu. Madereva walio wengi waliamua kukatiza kwenye service road ambayo, kwa bahati mbaya, nayo ilielemewa kupita kiasi. Magari yalikuwa hayaendi. Abiria wengine, kama anavyoonekana huyo mama hapo juu walichukua uamuzi wa kuachana na usafiri wa magari na kuanza kutembea, wakijihatarisha kwa kupita katika eneo ambalo usalama wa barabarani uliwekwa rehani.

Ninachojiuliza ni kuwa:

1. Hawa waliopitisha uamuzi wa kujenga daraja hili la matangazo saa hizo ambazo barabara hiyo inatumika sana walikuwa wakifikiri nini?

2. Je, kama wangeamua kufanya kazi yao hiyo usiku kuanzia saa 6 hivi, wangepoteza nini?

3. Je, kulikuwa na uharaka gani wa kufanya kazi hiyo mchana kweupe badala ya usiku?

Hebu tufikirie gharama waliyolipa watumiaji wa barabara hiyo:

1. Hakuna gari lililokaa chini ya nusu saa mahali hapo.

2. Hakuna gari lililozimwa kwa muda wote huo likiwa hapo, hii ina maana mafuta yaliendelea kuteketea.

3. Abiria na watumiaji wengine wa barabara walipoteza muda mwingi hapo, wengine wakiwahi kurudi majumbani na wengine wakielekea katika maeneo yao ya kazi au biashara.

4. Sijui kwa wasafiri wa ndege, inawezekana wapo waliokosa ndege zao kwa sababu ya kukosa mahali pa kupita, sina hakika kama kuna watu wa namna hii nani atawalipa fidia kwa hasara waliyoingia.

5. Kutokana na msongamano ulivyokuwa, si ajabu yapo magari mengi tu yaliyopigana pasi, hii ina maana hayana budi kufanyiwa matengenezo fulani ikiwa ni pamoja na kupakwa rangi sehemu yalipokwanguliwa.

6. Inawezekana kuna waliolizwa na vibaka kutokana na msongamano uliokuwepo wa magari, ninaamini tukitafuta tutapata taarifa za aina hiyo.

7. Uharibifu wa mazingira – hatuwezi kupuuzia, kulikuwa na uchafuzi mkubwa wa hali ya hewa mahali hapo kutokana na moshi wa magari na kelele zake, vile vile kule kupitapita kwa magari huku na huko madereva wakijaribu kupenya hapa na pale, kuna uharibifu uliotokea, hilo ni hakika.

8. Yote haya bila shaka yaligusa kwa kiasi fulani uchumi wa Taifa – mafuta ya magari, ununuzi wa rangi za magari kwa yale yaliyopigana pasi, vipuri, muda wa kazi na uzalishaji kutumika visivyo, miundombinu ya barabara kutiwa ubovu kutokana na vurugu hizo na menginenyo mengi, ambayo yote yanamaanisha matumizi ya fedha za kigeni ambazo Taifa linajipatia kupitia kuuza korosho, kahawa, tumbaku, pamba, mkonge, utalii na kadhalika.

Ipo haja kwa wakandarasi na wengine wenye kufanya uamuzi kupima na kuona athari za uamuzi wao kabla hawajautekeleza.

Kwa hitimisho, nampongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kusudio lake la kuwachukulia hatua za kinidhamu wale wote walioshiriki au kupanga au kutekelezwa au kwa yote mawili bomoabomoa ya Tabata Dampo, kitendo ambacho ni ukiukwaji wa haki za binadamu kwa kiwango cha juu sana.

Mungu ibariki Tanzania.


Posted in Siasa na jamii

Mambo ya lugha …

lugha111.jpg

Jamani, kuuliza si ujinga. Hivi hapa lugha imekaakaaje? Kila nikiipanga hainipi.

Hii ni katika barabara iendayo Kinyerezi kutokea Barabara ya Nyerere eneo la Majumba Sita. Kipande hiki kinafanyiwa matengenezo kwa sasa.


Posted in Siasa na jamii

Kipunguni to Kitunda

bananakitunda.jpg

darajakitunda2.jpg

Hili ni daraja linalounganisha eneo la Kipunguni na lile la Kitunda ukitokea eneo la Banana, jijini Dar es Salaam. Bila shaka litakuwa kiungo muhimu katika eneo hili, hasa nyakati za mvua. Wasiwasi wangu ni kuhusu uimara wake. Mimi siyo injinia, lakini nikitazama ujazo wa hizo nondo zilizotumika kusuka daraja hili, ninapatwa na wasiwasi. Je, litadumu? Au labda niulize, life span ya daraja hili imekusudiwa kuwa miaka mingapi?


Posted in Siasa na jamii

Mabango, foleni … mitaani

mabangokigogo.jpg

magomenitokigogo.jpg

kinondonimbuyunidar.jpg

Ni tarehe 1 Machi 2008. Barabara ya Kawawa: Kinondoni Mkwajuni, Magomeni (eneo la Mikumi kushuka bonde la kuelekea Kigogo) na karibu na Round About ya Kigogo.

Kuna mengi ya kufanya ili kufikia standards zinazokubalika. Picha zinaeleza mengi.


Posted in Siasa na jamii
Next Page »

About author

I am a citizen of Tanzania. I live in Dar es Salaam, commercial city of Tanzania. I am an editor, particularly dealing with books as well as other publications and related activities: editing, translating, supervising design and layout, monitoring printing, warehousing and dissemination of the books. I am also an author: I write children's story books, school textbooks and adult books. I undertake translation tasks from English to Kiswahili and vice versa. I do book indexing, that is preparing an index for a professional book. Contact: kakasimba@gmail.com . Feel free to get in touch with me.

Search

Navigation

Categories:

Links:

Archives:

Feeds