Nchi za Afrika ya Mashariki zipo katika mchakato wa kuelekea kuunda shirikisho lao. Wahenga walisema ‘umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu’. Kwa mantiki ya msemo huo, lengo la kuunda Shirikisho la Afrika ya Mashariki ni jema, ni zuri.
Katika siku za hivi karibuni, nchini Tanzania kuna Kamati ya Prof Wangwe inayofanya kazi ya kuratibu maoni ya wananchi juu ya namna gani mchakato wa uundaji huu ufanyike kwa kasi zaidi. Watu wengi waliopata fursa ya kutoa maoni yao juu ya suala hili wamesema hapana. Shirikisho la Afrika ya Mashariki, hapana. Sababu walizotoa ni nyingi, baadhi yake ni:
1. Uchumi wa Tanzania haujakomaa kiasi cha kutosha kuingiliana vyema na chumi za wenzetu katika namna itakayowanufaisha Watanzania.
2. Kuundwa kwa shirikisho kutamaanisha kukaribisha pia matatizo (has ya kijamii na kisiasa) kutoka katika nchi za wenzetu – matatizo ambayo kwa kiasi kikubwa Tanzania imekwishayamaliza kwa upande wake.
3. Katika nyanja ya uchumi – kuna uwezekano mkubwa kuwa Watanzania ndiyo watakaokuwa wapoteazaji, maana si Watanzania wengi wenye elimu ya juu kama wananchi wa mataifa ya jirani, hivyo, ajira itakuwa ni tatizo kwa Watanzania, ikitangazwa nafasi ya kazi basi ni Watanzania wachache tu watakaokuwa na sifa za kuishindania, matokeo yake, Watanzania watabaki kushika nafasi za chini kama vile za ufagizi wa ofisi, kufyeka nyasi, uhudumu ofisini na ulinzi (katika kampuni ambazo hata ulipaji wake ni wa matatizo).
4. Sambamba na hilo la uchumi, watoa maoni wengi wanabashiri kuwa kutazuka migogoro katika upande wa ardhi. Kwa sababu ya uhaba wa ardhi katika baadhi ya mataifa tunayokusudia kujiunga nayo, wananchi wengi kutoka kule wataingia Tanzania na kuwa na haki ya kumiliki ardhi, hapo kutakuwa na mgongano na Watanzania ambao kwa kiasi kikubwa ardhi haikuwa tatizo kwao.
5. Sababu za kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, awamu ya kwanza, mwaka 1977 bado hazijawekwa wazi kiasi cha kutosha. Na ikiwa sababu zile bado hazijatafutiwa ufumbuzi na uchambuzi yakinifu, iweje leo liundwe shirikisho ambalo ni hatua ya mbele zaidi ya jumuiya?
6. Watoa maoni wengi bado hawajaridhishwa na namna hatua mbalimbali za kuelekea kwenye shirikisho zinavyoendeshwa, yaani ushiriki wao ni duni katika hili.
7. Na sababu nyingine nyingi.
Kwa kutazama mambo hayo hapo juu, nashawishika kusema kuwa ingawa ‘umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu’ bado mataifa haya ya Afrika ya Mashariki hayajakomaa kiasi cha kuunda shirikisho au umoja.
Ninashawishika kufikia hitimisho hilo kwa kujikita katika hoja ya sababu za kushindwa kwa jumuiya ya Afrika ya Mashariki, awamu ya kwanza, na namna ambavyo jumuiya hivyo iliparaganyika. Katika literature mbalimbali zinazozungumzia juhudi za kufufua Jumuiya ya Afrika ya Mashariki hakuna mahali ambapo matatizo yaliyosababisha kuvunjika kwa jumuiya awamu ya kwanza yameshughulikiwa kikamilifu.
Ni ukweli kwamba jumuiya ya awamu ya kwanza ilidumu muda wa miaka 10 tu. Ni ukweli kwamba jumuiya ile ilianguka vibaya. Ni ukweli kwamba kulikuwa na ‘maumivu’ makali kwa pande zote na athari zake bado zingalipo hata leo (Wastaafu wa Jumuiya hiyo nchini Tanzania wamepata matatizo makubwa katika kulipwa mafao yao – ama kiduchu, au sababu ya kucheleweshwa wengine wameshatangulia mbele za haki huku wakiacha nyuma jasho lao). Si ajabu basi sababu ya kuvunjika kwa jumuiya ile kulichangia kuchochea kuibuka kwa vita vya Uganda ambavyo vimeyagharimu mataifa yaliyohusika fedha nyingi (athari zake bado zingalipo kwa uchumi wa Tanzania) na maisha ya watu wengi (combatants and non-combatants). Inawezekana kabisa kuwa matatizo ya Uganda (chini ya Amin wakati ule) yangeweza kabisa kumalizwa kwa njia nyingine zaidi ya vita.
Hivyo, kama walivyoshauri watoa maoni wengi wa Tanzania, wakati mwafaka kwa shirikisho haujafika. Utafika tu pale mataifa haya yatakapokuwa yamechunguza kiyakinifu na kwa kina sababu zilizosababisha kuvunjika kwa jumuiya ya awamu ya kwanza na kujishawishi kuhusu masuluhisho kwa matatizo yaliyotokea wakati ule. Hivyo, kipindi hiki ingefaa kitumike kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa yale yaliyojiri miaka hiyo ishirini na ushee iliyopita. Kwa uchache basi, shirikisho lifikiriwe kuundwa si chini ya miaka 25 kutoka sasa.
Ni kweli si WaKenya, WaGanda au WaTanzania tuliokuwa na mipaka ya mataifa haya kama tunavyoiona leo. Tulitenganishwa na wageni (wakoloni). Ipo haja ya kuungana. Lakini inabidi kuwe kuungana ambako kutatufaidia sote katika uwiano wa haki. Tuwaepushie wakazi wa eneo hili la Afrika matatizo yatakayosababishwa na papara ya kuunda shirikisho. Ikiwa matatizo yaliyosababishwa na kuvunjika kwa jumuiya ya awamu ya kwanza bado tunayahisi mpaka leo, basi tujue kuwa kuvunjika kwa Shirikisho kutakuwa na athari kubwa zaidi na mbaya zaidi.
Nachokoza.